|
Wakulima wa zao la pamba msipokee madawa yaliyochelewa
2006-10-24 14:09:29
Na Radio One Habari
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Brigedia Jenerali mstaafu Yohana Balele amewataka wakulima wa zao la pamba wasipokee madawa yaliyochelewa kutolewa na bodi ya pamba ili kuepuka hasara na usalama wa maisha yao.
Kauli yake inafuatia malalamiko ya wakulima wa zao hilo wilayani Maswa juu ya tabia ya bodi hiyo kuwapelekea madawa katika kipindi cha Aprili, Mei na Juni majira ambayo vitumba vya pamba huwa vimekomaa tayari kwa mavuno ya pamba na dawa kutotumika katika kipindi hicho.
Amesema ni hasara kwa mkulima kupokea madawa hayo katika kipindi ambacho hayatatumika na kwamba ni hatari kwa maisha na familia yake kukaa nayo ndani ya nyumba kwa vile madawa hayo ni sumu na yanahitaji utunzaji wa kifamasia.
Mkuu huyo wa mkoa wa Shinyanga alikuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na wakulima wa vijiji vya tarafa za Nhungu, Sengerema na Mwanga wilayani Maswa.
|