|
Auawa kwa kukatwa mapanga Kijiji cha Zigua Mamboleo
2006-12-31 15:48:16
Na Radio One Habari
Watu wenye silaha wamemuua mkazi mmoja wa Kijiji cha Zigua Mamboleo, wilaya ya Muheza, mkoani Tanga kwa kumkata mapanga wakati akiwa porini akichunga mbuzi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Bw. Brown Lekey amesema watu hao ambao hawafahamiki walimvamia Omar Shabani na kumuua siku ya Krismasi tarehe 25, mwezi huu.
Amesema taarifa za kuonekana kwa mwili wa Shabani zimetolewa katika kituo cha Polisi cha Muheza na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Omari Hamisi.
Bw. Lekey amesema kugundulika kwa mauaji hayo kulitokana na watu wanaoishi nyumba moja na Shabani kushtuka baada
ya kuona mbuzi aliokuwa akiwachunga wakirejea nyumbani peke yao.
Kaimu Kamanda huyo wa polisi mkoa wa Tanga amesema polisi kwa kushirikiana na wakazi wa eneo hilo la Zigua Mamboleo wanaendesha msako ili kuwanasa waliohusika na mauaji hayo.
|