|
Wavuvi wadogo kutumia raslimali kwa njia endelevu
2007-01-04 17:32:47
Na Radio One Habari
Wizara ya maliasili na utalii imesema itahakikisha sekta ndogo ya uvuvi inasimamiwa ipasavyo kuwezesha wavuvi wadogo kutumia raslimali ya uvuvi kwa njia endelevu na kwa ufanisi ili kuwaongezea kipato.
Katibu Mkuu wa Wizara Bwana Salehe Pamba amesema Tanzania imebahatika kuwa na maeneo mengi ya shughuli za uvuvi na ambayo yanaweza kuchangia katika vita dhidi ya umasikini.
Amesisitiza kuwa usimamizi kikamilifu utawezesha sekta ya uvuvi kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi hususani katika kuhakikisha lishe bora, utunzaji wa mazingira, kuinua pato la taifa, kuwapatia wananchi ajira na kipato.
Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa idara ya uvuvi Bwana PAMBA amesema uvuvi na biashara ya samaki ndiyo tegemeo kubwa zaidi kwa wananchi waishio kwenye maeneo ya uvuvi kuliko uzalishaji wa aina nyingine.
Kwa upande wa mwambao wa pwani amesema wanawake katika sekta hiyo pia wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika kilimo cha zao la mwani kuwanufaisha kuboresha maisha yao na kutoa huduma za mama lishe na maduka ya bidhaa mbalimbali.
|