|
Vyama vya Waajiri Barani Afrika vyapewa changamoto
2007-04-24 17:11:15
Na Radio One Habari
Tanzania imesema vyama vya waajiri barani Afrika vinaweza kutoa mchango mkubwa ikiwa vitaungana na serikali kukuza na kuhamasisha uwekezaji kwani ukuaji wa uchumi na uwekezaji ni pande mbili za sarafu moja.
Changamoto hiyo imetolewa mjini Addis Ababa, Ethiopia jana na Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati akifungua mkutano wa siku moja wa muungano wa Vyama vya Waajiri Barani Afrika.
Amesema inabidi mataifa ya Afrika yaongeze juhudi katika kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka ndani na nje katika uchumi wao, jambo ambalo linahitaji nguvu za pamoja kwa kushirikiana na serikali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari madhumuni ya kikao cha jana ilikuwa kuonesha mchango wa sekta binafsi na ule wa waajiri katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo, kuhakikisha kuwa serikali zinaweka mifumo ya kukuza na kutengeneza ajira.
Leo Rais Jakaya Kikwete atahutubia mkutano huo ambao unahudhuriwa na viongozi kadhaa wa Afrika, mabalozi wa nchi za Afrika walioko Addis Ababa, wawakilishi wa Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na washiriki mbalimbali duniani wanaoshughulika na maswala ya Ajira.
Rais atarejea nyumbani kesho.
|