|
Wazazi wa kitongoaji wa Milamba waomba shule
2007-04-29 15:21:47
Na Radio One Habari
Wazazi wa kitongoaji wa Milamba katika halmashuri ya wilaya ya Lindi wameiomba serikali kuwapatia huduma ya shule ya msingi ili kuwawezesha watoto wao kupata elimu.
Ombi la wazazi hao linafuatia kukosekana kwa huduma hiyo muhimu katika kitongoji hicho kilichopo kilomita 8 kutoka kijiji mama cha Malumbo.
Wazazi hao wametoa ombi hilo mbele ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Lindi Bwana Ahmad Mussa Mbonde kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kitongoji hicho kilichopo kata ya Mandwanga tarafa ya Nyangamara.
Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na afisa elimu wa halmashauri ya wilaya hiyo Bwana Minduva Hassan wananchi hao wamewahakikishia viongozi hao kuwa wako tayari kuchangia nguvu zao katika kufanikisha ujenzi wa shule hiyo endapo ombi lao litakubaliwa ili kuondoa kero hiyo.
Akizungumza na wananchi hao Bwana Mbonde ameahidi kulifikisha suala hilo katika vikao husika vya halmashauri yake na kuwataka wavute subira huku wakijiandaa kwa ajili ya ujenzi huo mara ombi lao litakapopitishwa.
|