|
Kundi kubwa la tembo limevamia mashamba na kufanya uharibu
2008-05-16 15:47:43
Na Radio One Habari
Kundi kubwa la tembo kutoka katika pori la hifadhi la Maswa limevamia mashamba na kuharibu hekta 90 za mazao mbalimbali ya wananchi katika wilaya ya Meatu mkoani Shinyanga katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Akitoa taarifa ya wilaya hiyo kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Ezekiel Maige, Mkuu wa wilaya ya Meatu Bwana Abihudi Saideya amesema tembo hao walivamia mashamba hayo kati Aprili mwaka jana na Aprili mwaka huu katika vijiji sita vya wilaya hiyo.
Bwana Saideya amesema tembo hao waliharibu mazao ikiwemo mahindi, viazi, miwa, mboga na matunda ambapo hasara iliyosababishwa na uharibifu huo bado haijafahamika na kwamba wananchi walioathirika watakabiliwa na uhaba wa chakula mwishoni mwa mwaka huu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Maige ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kuendelea kutoa elimu ya kuwataka wananchi kuacha kulima karibu na hifadhi hiyo.
|