|
Kizimbani Pemba yafuzu 8-Bora Zenji
2006-07-09 09:19:10
By Bahati Mollel
Wakati timu ya Jeshi la Kujenga Uchumi, JKU imeungana na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Zanzibar, Polisi, kucheza hatua ya nane-bora itakayoanza Agosti 25 kwenye uwanja wa Amaan, timu ya Kizimbani nayo imefuzu kutoka Pemba.
Katibu Mtendaji wa Chama cha Soka cha Zanzibar, ZFA, Mwinyijuma Saadat alisema kwa njia ya simu kuwa timu hizo zimefuzu baada ya kujikusanyia pointi 37 na 34, ambazo hazitaweza kufikiwa na timu yeyote kwenye kundi lao la B.
Saadat alisema kwa upande wa kundi A timu za KMKM na Mundu nazo zimetinga hatua hiyo kwa kujikusanyia pointi 32 kila mmoja, na haziwezi kufikiwa na timu za Small Simba na Malindi zenye pointi 23 na 22 huku zikiwa zimesaliwa na mechi mbili kila mmoja.
Tayari tumeshazipata timu nne za Unguja ingawa bado hatua ya makundi haijamalizika na tunasubiri za Pemba ili kukamilisha idadi ya timu nane, alisema Saadat.
Hata hivyo, alisema timu sita -- tatu kutoka kila kundi -- ambazo zipo katika hatihati ya kushuka daraja, zimezinduka na kufanya vyema katika mechi zao za hivi karibuni, ambapo katika kundi A Kipanga imejikusanyia pointi 15 huku Forodha na Urafiki zikifikisha pointi 13 kila mmoja, wakati katika kundi B Wales imekusanya pointi 17 sawa na Mtende Rangers, huku Kizimkazi ikilingana na Bandari kwa pointi 15.
Saadat alisema mechi za leo ni kati ya Small Simba kukwaana na Mafunzo kwenye uwanja wa Mao, wakati Mtende Rangers itacheza na Wales katika uwanja wa Amaan.
Naye Katibu Msaidizi wa ZFA Pemba, Asan Othuman Juma alisema kwamba kumekuwa na ushindani mkubwa wa kuwania nafasi ya kucheza hatua hiyo, ambapo timu pekee iliyofuzu ni Kizimbani yenye pointi 38, akifuatiwa na FSC, Mwenge na Chipukizi wenye pointi 23, 21 na 20 katika kundi A wakati katika kundi \B\ Duma inaongoza kwa kuwa na pointi 36, ikifuatiwa na Young Islanders na Hardrock zenye pointi 34 na 33.
Wakati huohuo, ZFA imewataka wadau wa soka visiwani huko kuwasilisha maoni yao mbalimbali ili kufanikisha maendeleo ya mchezo huo.
Saadat alisema maoni hayo yameanza kupokelewa kwenye ofisi za chama hicho na mwisho wa kuwasilisha ni Julai 10, ambapo yatawasilishwa kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi wa ZFA, ambao umepangwa kufanyika Julai 29.
Naye Katibu mkuu wa BMTZ, Mzee Zam Ally aliwataja wagombea tisa waliojitokeza kuwania nafasi za uenyekiti na umakamu kutoka Unguja na Pemba, kuwa ni Ali Fereji Tamim na Shafi Mussa (uenyekiti); Farouk Karim, Yussuf Chunda, Haji Ameir, Ramadhani Khalifan na Salehe Zam (Makamu Unguja); Suleiman Amour na Mohamed Said (Makamu Pemba). Mwisho wa kuchukua fomu ni Julai 12 wakati usaili ni Julai 21.
|