09 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

TFF yatakiwa kuunda ’TFF-Dada’
 
2006-07-09 09:20:09
By Mwandishi Wetu

Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, imetoa ushauri wa bure kwa Shirikisho la Soka nchini, TFF, kuanzisha chama cha soka cha wanawake, ili kukuza mchezo huo ambao unatamba duniani kwa sasa.

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Waziri Mohammed Seif Khatib jijini ambapo alisema kama soka la wanawake litapata uongozi wake wa kuliendesha, litakuwa na mikakati mbalimbali ya kimaendelea ikiwemo ya kuendesha ligi zao mbalimbali likifuata taratibu zitakazowekwa na TFF.

Mbali na wanawake, pia Khatib ametaka kuanzishwa kwa chama cha soka kwa vijana wadogo ili kukuza soka nchini.

’’Hakuna ubaya kwa vyama hivi kuanzishwa kwani vitakuwa vinapunguza majukumu kwa TFF, ambayo inaonekana kuelemewa na kazi ya usimamizi wa soka ya wanawake na vijana,’’ alisema Khatib.

Kwa sasa soka la wanawake linaongozwa na uongozi wa muda, wakati kwa vijana hakuna uongozi zaidi ya wenye shule binafsi kuungana na kuunda umoja wao unaowatambulisha na kuandaa mashindano mbalimbali.

Waziri aliwataka watu mbalimbali kuanzisha shule za mchezo wa soka, ikiwa ni pamoja na kuomba kuwepo kwa somo la michezo katika shule za serikali ambalo anaamini kwa kutiliwa mkazo, litainua viwango vya michezo nchini.

Aliongeza kuwa wizara yake itaandaa mjadala wa kitaifa wa kuzungumzia masuala ya michezo nchini, ambao utafanyika baadaye mwezi ujao baada ya kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo katika bunge la bajeti linaloendelea sasa mjini Dodoma.

’’Huu mjadala utahudhuriwa na Rais Kikwete ambaye tayari amekubali na kutakuwa na nafasi kubwa kwa wadau na watu mbalimbali kuzungumzia jinsi ya kuboresha michezo kwa ujumla nchini,’’ alisema Khatib.

Timu za Taifa za Tanzania zimekuwa zikiboronga katika michuano mbalimbali ya kimataifa kutokana na kuwa na maandalizi duni na kukosa makocha wenye sifa, ambapo hivi karibuni serikali imemtangaza kocha Marcio Maximo kutoka Brazili kuwa miongoni mwa makocha wawili watakaokuja kuzinoa timu za wakubwa na vijana za soka.

  • SOURCE: Lete Raha
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.