|
Timu ligi kuu zaponda usajili mpya
2006-07-09 09:21:56
By Bahati Mollel
Timu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara, zimeponda utaratibu wa TFF wa kuongeza wachezaji kwa ajili ya mzunguko wa pili, zikisema hauna maana kutokana na shirikisho hilo la soka nchini kuchelewesha bila ya sababu kuwaidhinisha wachezaji walioongezwa ili watumike.
Mlezi wa timu ya Kagera Sugar, Mohamed Hussein alisema kuwa usajili huo ulitakiwa kupewa muda mrefu na kuanza mapema, ili kutoa nafasi kwa timu kuweza kuwatumia wachezaji waliwaongeza wakati mzunguko huo utakapoanza.
Hussein alisema wamesajili wachezaji wapya kwa gharama kubwa na wanaendelea kuwahudumia kwa kuwa tayari ni mali yao, lakini hawawezi kuwatumia hadi watakapoidhinishwa na kamati ya ligi ya shirikisho hilo.
TFF imesema itawaidhinisha wachezaji hao Julai 15.
Hii inakuwa haina maana kwani wachezaji tunawasajili kwa ajili ya mzunguko wa pili, lakini mechi zinaanza na hatutawezi kuwachezesha hadi wapitishwe, sasa kwa nini wasingetoa muda mrefu kabla ya ligi kuanza ili ligi inapoanza tu wawe tayari kutumika? alihoji Hussein.
Kagera ambayo imekiri kuwa ina matatizo katika nafasi ya ushambuliaji, imewaongeza wachezaji wa zamani wa Yanga, Omar Chan\ga na Yussuf Macho \Musso\, ambao walionyesha uhai katika nafasi hiyo kwa kucheza vizuri katika mechi za kirafiki zilizofanyika Zanzibar.
Naye Kaimu Mkuu wa Kahama United, Martin Maige aliungana na Hussein kuuponda utaratibu huo. Timu yake imewasajili wachezaji Chesido Methew na Idd Juma, lakini wameshindwa kuwatumia katika mchezo wao wa kwanza wa mzunguko wa pili dhidi ya Polisi Dodoma Jumatano na kusababisha kuchapwa magoli 3-1.
Kwa upande wa Simba ambao wataanza hatua hiyo Julai 16 kwa kuumana na Bandari Mtwara, Kocha Mkuu, Neider Dos Santos alisema wameongeza wachezaji watano na wanasubiri TFF kuwaidhinisha ili waanze kuwatumia. Lakini Simba huenda ikakatwa nafasi moja kwa kuwa ilikuwa na nafasi nne za kusajili ili kufikisha idadi ya wachezaji 30.
Simba imewaongeza Shabaan Kisiga, Sadick Muhimbo, Ali Itahi, Sio Zinapio na Mohamed Hanzuruni baada ya kuwatema Christopher Alex, Salum Mpakala na Rexine Ongoli, wakati Yanga kwa mujibu wa kocha mkuu Jack Chamangwana wamewaongeza Hilary Chesa na Emmanuel Swita. Nao walikuwa na nafasi moja ya kusajili.
Utaratibu huo wa kuongeza wachezaji ulianza wiki moja iliyopita na mwisho kuwa Julai 4, lakini wanalazimika kusubiri siku saba za pingamizi kama litakuwepo dhidi ya mchezaji na baada ya hapo kamati ya ligi itapitia na kuwasilisha mapendekezo yake kwa kamati ya utendaji ambayo itakutana Julai 15 kuidhinisha kutumika kwa wachezaji hao.
|