|
Ulimboka si mtovu Stars, auguliwa na mama
2006-07-09 09:22:45
By Bahati Mollel
Mshambuliaji nyota wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Ulimboka Mwakingwe amesikitishwa na taarifa za kocha mkuu wa timu hiyo, Mshindo Msolla za kudai amemuondoa katika kikosi hicho kwa utovu wa nidhamu.
Ulimboka amesema jijini kuwa alimtaarifu Msolla na meneja wa timu hiyo, Titus Bandawe kuwa ana matatizo ya kifamilia, hivyo hataweza kuwemo katika kikosi hicho kilichokuwa kikienda Shelisheli kucheza mechi za kirafiki za kimataifa za kusherekea miaka 30 ya Uhuru wa nchi hiyo lakini ameshangazwa na kilichosemwa na kocha huyo dhidi yake.
Nilifika pale hosteli na kusaini kitabu nikiwa ni mchezaji wa 16 kati ya 20 waliokuwa wameitwa, lakini kutokana na matatizo ya kumuuguza mama yangu mzazi, nikawaomba waniondoe katika safari ili nisizibe nafasi ya mchezaji mwingine na wakakubali kuwa nina matatizo ya kifamilia, alisema.
Uli anamuuguza mama yake mzazi mwenye matatizo ya kibofu cha mkojo, na Jumamosi iliyopita alikuwa katika hospitali ya Agakhan akichukuliwa vipimo mbalimbali, ili baadaye aweze kufanyiwa upasuaji, ambao utakuwa ni mara ya pili, ambapo awali alifanyiwa mwezi Januari mwaka huu.
Hata hivyo, Msolla alipoulizwa juu ya sakata hilo, hivi karibuni alisema walishindwa kumvumilia Ulimboka kwa siku tatu akiwa nje ya kambi kwa kuwa na matatizo, na kuamua nafasi yake wampe mchezaji mwingine.
Kila chombo cha habari kinaripoti kinavyojua, sisi tulisema Ulimboka ameondolewa na nafasi yake ilichukuliwa na Mwaikimba, na sio mtovu wa nidhamu.
Tusingeweza kumuweka katika timu kwa wakati ule kwani angekuwa hajafika katika mazoezi kwa siku tatu, alisisitiza Msolla.
Alisema Ulimboka aliomba kuwa nje ya mazoezi kwa siku mbili, na baadaye aje kuungana na wenzake watakaokwenda Shelisheli, lakini ilishindikana kwa kuwa angekuwa hana mazoezi ya kutosha.
Katika hatua nyingine, Msolla alisema kuwa kwenye ripoti yake ya mazoezi, kambi na safari ya Shelisheli atakayoiwasilisha kwenye Shirikisho la Soka, TFF, kesho Jumatatu, kutakuwa na majina ya wachezaji watatu atakaowatema kwa kushuka kiwango na kuongeza wengine watatu wa nafasi ya kiungo na ushambuliaji.
Alisema wanatarajia kuanza tena kambi Jumatano ijayo kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Rwanda, ambayo itafanyika Jumamosi ijayo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Stars ambayo inajiandaa na mechi za kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa kuumana na timu za Burkina Fasso, Senegal na Msumbiji, ilishinda mchezo mmoja dhidi ya Madagascar 2-1 na kufungwa na Shelisheli 2-1, ambapo Msolla amesifia kiwango cha juu cha wachezaji wake, ingawa alisema ameona mapungufu katika nafasi za kiungo na ushambuliaji.
|