|
Yanga yabanwa mbavu Mtibwa
2006-07-09 09:23:50
By Bahati Mollel, Morogoro
Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga jana walipunguzwa kasi katika kampeni zao za kutwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom, baada ya kutoka suluhu na Mtibwa Sugar katika mchezo wa ligi hiyo uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Yanga ilifanya shambulizi la nguvu katika dakika ya sita baada ya Mkenya John Barasa kupiga shuti lililookolewa na kipa Sudi Slim wa Mtibwa, lakini timu hiyo ilipata pigo muda mfupi baadae baada ya Barasa kupigwa kipepsi na kukimbizwa hospitali ya mkoa ambako amepumzishwa kwa matatibabu zaidi.
katiKa dakika ya 19, Shadrack Nsajigwa nusura afunge kufuatia kona ya Gaudence Mwaikimba, lakini alipiga nje mpira huo.
Said Maulid wa Yanga SMG nusura afunge katika dakika ya 32 lakini akiwa katika nafasi nzuri, alipiga nje, huku Mtibwa Sugar ikajibu mapigo katika dakika ya 37 baada ya Nizar Khalfan kukosa bao la wazi.
Yanga iliibuka tena katika dakika ya 44 wakati Abuu Ramadhani aliyeingia badala ya Barasa katika dakika ya 27 alipiga shuti kali lililookolewa na kwa kichwa na Mecky Maxime, huku timu hiyo ikosa tena mabao kupitia kwa Nsajigwa na maulid katika dakika ya 50 na 57.
Kwa suluhu hiyo, Yanga sasa imefikisha pointi 39 baada ya kucheza mechi 16, ikashinda 12, ikatoka sare tatu na kushindwa moja, huku Simba ambayo jana haikuingia uwanjani bado inaendelea kuwa ya pili kwa kuwa na pointi 31.
Kocha wa Mtibwa Mkenya James Sianga aliendelea kulalamikia waamuzi, ambapo alisema kuwa mwamuzi Idd Manase wa Dodoma aliiuma timu yake kwa kupiga ovyo filimbi za kuotea kila washambuliaji wa Mtibwa wanapolikaribia lango la Yanga.
Mtibwa Sugar:Sudi Slim, Mecky Mexime, Amir Maftaha, John Mabula, Ibrahim Mwaipopo, Shaban Nditi, Zuberi Katwila/Said Mkopi (63), Abdi Kassim, Abdallah Juma, Aboubakar Mkangwa/Sammy Kessy (84) na Nizar Khalfan.
Yanga:Benjamin Haule, Shadrack Nsajigwa, Fred Mbuna, Nadir Haroub, Lulanga Mapunda, Edwin Mukenya, Mohamed Banka/Waziri Mahadhi (80), Amri Kiemba, Said Maulid SMG, John Barasa/Abuu Ramadhani (27) na Gaudence Mwaikimba/Heri Moris (70).
Mwandishi wetu anaripoti kutoka Mlandizi mkoani Pwani kuwa;Twiga Sport ya jijini Dar es Salaam jana iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao Ruvu Shooting, huku bao hilo pekee likifungwa na Paul Ngwai katika dakika ya 45 baada ya kuunganisha mpira wa adhabu.
Naye Samson Barnabas wa PST Mbeya, anaripoti kuwa;Prisons ya huko jana ililazimishwa sare ya 1-1 na Bandari Mtwara katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Sokoine, huku wageni wakiwa wa kwanza kupata bao walilofunga kwa njia ya penati katika dakika ya 23 na Prisons walisawazisha katika dakika ya 47 mfungaji ni Oswald Morios pasi ya Yona Ndabila.
Mwandishi Wetu anaripoti kutoka Uwanja wa taifa wa Dar es Salaam kuwa;Polisi Morogoro jana iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Transit Camp.
Kutoka Dodoma, Mary Edward anaripoti kuwa;Polisi ya huko jana iliibuka na pointi zote tatu baada ya kuifunga Kagera Sugar kwa bao 1-0 bao hilo likifungwa na Bantu Admin baada ya kutokea piga nikupige katika lango la Kagera.
Mchezaji wa Polisi Dodoma Noel Msako alipewa kadi nyekundu katika dakika ya 61 baada ya kumchezea vibaya Omary Ally.
|