|
20 kushuka daraja Zanzibar 2007
2006-12-24 09:23:18
By Mwandishi Wetu
Jumla ya timu 20 zitashuka kutoka ligi kuu ya Zanzibar msimu ujao, kwa mujibu wa chama cha soka cha huko, ZFA.
Timu 20 zitashuka daraja mwakani ikiwa ni mkakati wa kuwa na mfumo mpya wa ligi ambao utakuwa na timu 12 za ligi kuu Zanzibar ifikapo mwaka 2008.
Afisa Habari wa chama cha soka cha Zanzibar, ZFA, Maulid Hamad alisema katika mazungumzo kwa njia ya simu kuwa katika ligi kuu ijayo timu 10 za kanda ya Unguja zitashuka kucheza daraja la kwanza kanda mwakani na idadi kama hiyo ya timu za Pemba pia itapungua.
Maulid alisema timu hizo zitatokana na timu 16 zitakazoshiriki ligi za kanda mwakani katika msimu ambao utaanza Januari 25.
Kwa kushuka timu 10 za Unguja na 10 za Pemba, kutabakiza timu sita kila kanda ambazo zitacheza ligi kuu ya Zanzibar ambayo itakuwa moja mwaka 2008. Alisema kuanzia mwaka 2009 itakuwa ikishuka timu moja ya Unguja na moja Pemba, na kupanda idadi kama hiyo kutoka katika ligi za Kanda.
Pia alisema ligi za Kanda zitashirikisha timu 12 zikiwa ni 10 zilizoshuka daraja na mbili zitapanda kutoka daraja la Pili Kanda.
Tayari timu zimeanza zoezi la uhamisho wa wachezaji lililoanza Desemba 4 na litamalizika Jumatano, alisema Maulid na kuongeza kuwa usajili rasmi utaanza Januari Mosi hadi 14, na kutakuwa na timu 14 za pingamizi zitakazoanzia Januari 15-28.
Ligi kuu ya Zanzibar mwaka huu ilishirikisha timu 40, ikiwa 20 za Unguja na idadi kama hiyo za Pemba, baada ya aliyekuwa Waziri wa michezo, Haruni Suleiman kupinga kushushwa kwa timu tatu kwa mujibu wa kanuni, na kusababisha zibakizwe.
|