|
Yanga yailaumu TFF kutosogezwa Kagame
2006-12-24 09:25:32
By Mwandishi Wetu
Mabingwa wa soka wa Bara Yanga wamewataka viongozi wa shirikisho la soka, TFF, kuwa na desturi ya kutetea wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, kwenye mikutano ya Baraza la Mashirikisho ya Soka ya nchi hizo, CECAFA, wakati wa upangaji wa ratiba ya michuano.
Kaimu katibu mkuu wa Yanga Abdul Sauko alisema juzi Ijumaa viongozi wa TFF wanatakiwa kutetea wawakilishi wa nchi kwa kuwasilisha kalenda ya matukio ya soka ya Bara kwenye mikutano hiyo ili tarehe za mashindano ya CECAFA zisiingiliane na ya hapa nchini.
Sauko alisema kuwasilisha kalenda ya matukio mapema kunaweza kusaidia CECAFA kuona umuhimu wa kupanga kalenda yake mbali na mashindano ya nchi wanachama.
TFF wasiende kule kama wasindikizaji tu. Wawe wanatutetea sisi ambao ndio tunashiriki kwani bila kuweka muda muafaka wa mashindano timu zitakuwa zikicheza mfululizo na wachezaji wanahitaji kupumzika, alisema Sauko.
Alisema ratiba ya sasa ya michuano hiyo iliyopangwa kuanza Januari 6 kwa pamoja na Ligi ya Klabu Bingwa ya Afrika inayoanza Januari 26 vinaingiliana na mashindano ya Kombe la Taifa ligi ndogo. Karibu kikosi kizima cha Yanga kipo kwenye timu za mikoa mbalimbali zinazocheza Kombe la Taifa.
Yanga ilipendekeza kwa TFF kuahirishwa kwa Kombe la Kagame lakini CECAFA ilipinga ombi hilo kwa maelezo kuwa maandalizi ya michuano hiyo nchini Rwandsa yapo katika hatua za mwisho.
Katika hatua nyingine, TFF imesema ipo tayari kutoa msaada wa kiufundi kwa wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya klabu ya Afrika, timu za Yanga na Simba, endapo wataombwa kufanya hivyo.
Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela alisema jana Jumamosi endapo timu hizo zitahitahiji msaada ziandike barua kwenye shirikisho hilo ili ziweze kupata msaada.
Sisi hatutapenda wawakilishi wetu wakafanye vibaya, kama wanahitaji msaada wetu watutaarifu mapema tutawapelekea wataalam wa kiufundi na mahitaji mengine yaliyopo ndani ya uwezo wetu, alisema Mwakalebela.
Yanga itacheza na timu ya AGSM ya Visiwa vya Comoro katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwishoni mwa mwezi ujao wakati Simba itakutana na Textile du Pungue ya Msumbiji katika raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho la Afrika kati ya Januari 26-28, mwakani.
|