24 Dec 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Yanga walaumu uongozi kumuacha Wasso
 
2006-12-24 09:26:11
By Mwandishi Wetu

Baadhi ya wanachama wa Yanga wameulaumu uongozi wa klabu hiyo kwa kumuacha beki namba tatu Ramadhani Wasso bila sababu za msingi na kushindwa kusajili mchezaji wa kuziba pengo lake.

Wakizungumza na Lete RAHA jijini mwishoni mwa wiki kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini kwa hofu ya kuchukiwa na viongozi, wanachama hao walisema Yanga ya mwakani itakuwa na uchochoro upande wa kushoto wa beki.

Wanachama hao walisema baada ya uongozi kumuacha Wasso ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Burundi, Yanga imebakiwa na Abuu Ntiro tu kama mchezaji wa kuaminika katika nafasi hiyo na beki mwenyewe si tegemeo.

Walisema Ntiro ana tatizo kubwa la majeruhi hivyo bila ya kuwa na mchezaji mwingine wa kuaminika katika nafasi hiyo timu pinzani zinaweza kugundua udhaifu katika wingi ya kulia na kutumia upande huo kusababisha mashambulizi mfululizo Yanga.

Yanga hatahivyo imemsajili Emmanuel Swita kutoka Kahama United ya Shinyanga katika nafasi hiyo, lakini wanachama hao walio karibu na uongozi wamepinga wakisema ana udhaifu mkubwa katika kukaba ingawa ni mzuri katika kupanda.

Uzuri wa mchezaji huyo katika kupanda, inawezekana, ndiyo sababu kubwa ya Yanga kumsajili kwani kwa mfumo wa uchezaji wa Yanga wa 3-5-2, jukumu kubwa la mabeki wa pembeni ni kuongeza mashambulizi.

’’Hawa (viongozi) walimuona mara mbili tu katika mechi wakamsajili,’’ alisema mmoja wa wanachama hao na kuendelea, ’’lakini hakabi kabisa. Yeye ni kukimbiza tu mpira na hapo ni tatizo jingine kubwa, lazima asajiliwe mchezaji mwenye sifa zote na mwenye maamuzi ya haraka; sio huyu.’’

Walisema usajili ulipaswa kufuata mapendekezo ya makocha Jack Chamangwana na Sekilojo Chambua lakini badala yake viongozi wamejichukulia tu wachezaji.

’’Huyu Wasso aliachwa kwasababu ya kugombana tu (Meneja Robert) Ekerege. Tangu hapo akawa anapigwa benchi lakini si mchezaji wa kuachwa,’’ alisema mwanachama mwingine.

Wasso aliwahi kumlalamikia kwenye vyombo vya habari Ekerege kwa kutompa malipo yake ya posho ya shilingi 10,000 wakati timu ikiwa Mwanza na kwa kitendo hicho beki huyo mfupi alisimamishwa kwa muda kabla ya kusamehewa lakini hakuwa tena chaguo la kwanza katika nafasi ya beki namba tatu.

Usajili wa Yanga uliokwenda kwenye shirikisho la soka la Afrika, CAF, ni walinda mlango Ivo Mapunda, Benjamin Haule na Jackson Chove na mabeki Hamis Yussuf, Shadrack Nsajigwa, Fred Mbuna, Nadir Haroub ’Canavaro’, Lulanga Mapunda, Abuu Mtiro, Amir Maftaha na Wisdom Ndlovu.

Wengine ni Edwin Mukenya, Waziri Mahadhi, Amri Kiemba, Credo Mwaipopo, Emmanuel Swita, Abdi Kassim, James Chilapondwa ambao ni viungo.

Washambuliaji ni Said Maulid, Gaudence Mwaikimba, Abuu Ramadhani, Benny Mwalala, John Barasa, Thomas Maurice, Mrisho Ngassa, Gulla Joshu na Hussein Swedi.

Wachezaji waliotemwa pamoja na Wasso ni Deo Lucas, Andrew Carlos, Mohamed Banka, Kudra Omari, Mbaruku Suleiman, Salim Ahmed ’Mkweche’, Salum Athuman na Heri Morris.

  • SOURCE: Lete Raha
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.