27 Apr 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

CHID BENZ: Mwana-hiphop asiyeogopa kuitwa bishoo kwavile ni bishoo haswa
 
2008-04-27 09:56:47
By Amour Hassan

Sauti yake imetawala hivi sasa katika vituo vya radio nchini kiasi kwamba unaweza kumsikia zaidi ya mara NANE kwa siku katika kituo kimoja cha radio bila ya kurudiwa kwa wimbo uliosikia mara ya kwanza.

Unaweza kujiuliza hali inakuwaje katika Bongo hii iliyojaa vituo vya radio za FM ambavyo muziki wa kizazi kipya huchukua sehemu kubwa ya nyimbo zinazopigwa kwa siku.

Ni kwasababu mkali huyu wa hip hop anatawala Bongo hivi sasa.

Nyimbo zaidi ya NANE zilizo katika chati ya juu hivi sasa nchini zinahusisha sauti yake.

Wasanii wakali wa kizazi kipya na wanaochipukia, wote wanaonekana kuvutiwa na uwepo wake katika nyimbo zao.

Ngoma zinazotamba katika chati kama `Tamani` wa msanii aitwaye Tunda, `Bado Umenuna` wa Marlow, `Ombi Langu` wa memba anayeinukia kutoka kundi la Tip Top Connection aitwaye Spark, `Mchizi Wangu remix` wa kundi la Nako2Nako Soldiers, \'Hapo Sawa remix` wa Profesa Jay na \'Hao\' wa Mwansiti, zote zimemhusisha Chid.

Wimbo `Hawachani` wa nyota wa zamani wa kundi la Cocacola Popstar Langa Kileo wenye kiitikio kisemacho ``Ninaposimama Hawasimami, Ninapochana Hawachani`` pia umemhusisha Chid Benz, ambaye pia anatamba na nyimbo zake binafsi za albam yake kama `Hasira za Nini`, `Mmenisoma` na aliomshirikisha mwanadada K-Lynn, `Naitwa Nani`.

BISHOO HASWAA
Mshindi wa tuzo ya Msanii Bora wa Hiphop 2007, Chid anasema kinachotokea sasa kwake katika gemu ya kizazi kipya, ni safari tu.

``Ni safari tu,`` alisema rapa huyo juzi Ijumaa alipozungumza na Lete RAHA.

``Katika maisha ya kimuziki vinatokea vitu kama hivi… ni kama safari tu.

``Watu wametokea kuipenda tu sauti yangu kipindi hiki na wasanii wamejikuta wakiipenda tu. Ndio maana naitwa kufanya `featuring` nyingi.``

Rapa huyo aliongeza kuwa haamini maoni ya baadhi ya watu wanaodai kwamba kufanya kazi na wasanii wengi kutaifanya sauti yake ichokwe haraka masikioni.

``Kitu muhimu ni ujumbe mzuri katika kila wimbo unaofanya… sauti itachokwa kama utalazimisha kurekodi katika kipindi ambacho umeishiwa mistari.

``Mimi sikubali jambo hilo linitokee, narekodi pale tu ninapoamini kuwa nina mistari yenye ujazo itakayoufanya wimbo ubambe, sio kurekodi wimbo ilimradi tu,`` alisema Chid ambaye miongoni mwa mistari yake inayochangamsha katika wimbo wa `Hawachani` wa Langa ni ule usemao: ``Wanasema mi bishoo, yeah, mi bishoo haswaa``.

BENZINO/LA FAMILIA
Chid, ambaye jina lake halisi ni Rashid Abdallah, amesema baada ya kuingiza sokoni albam yake ya `Chid Benz` Februari, hivi sasa anashughulikia kuwatoa memba wa familia aliyoiunda chini yake ya La Familia.

``La Familia ina memba kibao wa fani tofauti. Kuna wasanii wa Hiphop, Bongofleva, mpira wa kikapu, soka na kadhalika.

``Kwa sasa tunaangalia kuwatoa memba wetu wa muziki wa kizazi kipya,`` alisema Chid, ambaye aliamua kulipunguza jina lake ili lisiendelee kufanana na la rapa Benzino wa Marekani ambaye pia ni mmoja wa wamiliki wa jarida la The Source lililokuwa na uhasama wa muda mrefu na rapa Eminem.

Chid amekuwa akilitaja sana jina la familia yake hiyo katika nyimbo zake nyingi anazoshiriki.

Itikadi za mwanahiphop huyo za kutowaponda wasanii wa kizazi kipya, tofauti na ilivyo kwa wasanii wengi wa hiphop, bila ya shaka zimechangia kuwavuta wasanii wengi kupenda kumshirikisha.

Miongoni mwa nukuu zake maarufu juu ya utata wa malumbano ya `ipi hip hop na ipi Bongofleva` ni iliyopata kuandikwa na safu hii wakati alipozungumza kwa mara ya kwanza na Lete RAHA Agosti 2006.

Huku akiheshimika kwa mashabiki kama msanii mgumu wa hip hop, Chid alisema: ``hakuna hip hop Bongo`` kauli ambayo ilibeba kichwa cha habari cha makala yake katika safu hii.

Katika makala yake hiyo Chid alisema: ``Hip hop ni utamaduni wa watu na huwezi kuuiga kwa kuwa utamaduni hauigwi.

``Utashangaa kuona mtu anasema yeye ni msanii wa hip hop wakati `beats` zake zina midundo ya rhumba kabisa... hiyo si hip hop.

Muziki wetu hauwezi kuwa hip hop kwavile una mapungufu mengi na kila chenye upungufu hakiwezi kuwa kitu halisi… lazima kitapewa jina jingine.

``Hata ukifotoa karatasi ya barua, itaitwa `kopi ya barua\' na wala si barua `original` tena, hivyo mtu hapa nchini hawezi kusema anafanya hip hop halisi... labda wakitaka waongeze jina jingine kuitambulisha aina ya hip hop wanayofanya.

``Wenzetu wa Afrika Kusini wana `Hiphop-Kwaito`. Hiyo inatokana na kutambua kuwa hip hop wanayofanya kuwa haiwezi kuwa halisi kama ya Marekani, na kwa kuwa Kwaito ndiyo inayotambulisha muziki wao wa vijana, ndio maana wakaamua kuunganisha majina hayo miwili kutoa aina yao ya muziki.

``Na hapa Bongo ni hivyo hivyo, hatuna hip hop halisi hapa. Labda tuiite hiphop yenye fleva za Kibongo, ambayo pengine itaishia kuitwa Hiphop-Bongofleva.``

  • SOURCE: Lete Raha
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.