|
Swedi:Mkali wa Simba anaedaiwa `kususia` mechi na Yanga
2008-04-27 09:57:39
By Ramadhani Mbwaduke
Kuna habari kuwa njaa na mkwara wa kufungiwa kwa kila mchezaji anayejaribu kutetea maslahi yake Simba ni baadhi ya sababu zitakazomfanya mlinzi Said Swedi wa `Wekundu wa Msimbazi` asiwepo hata katika orodha ya wachezaji wasiovaa jezi wa timu hiyo wakati watakaposhuka kwenye dimba la Uwanja wa Taifa kwa nia ya kuendeleza rekodi yao ya ushindi dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga.
Swedi ambaye ni miongoni mwa wachezaji sita waliojadiliwa jioni ya Alhamisi iliyopita kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu na kisha kunusurika baada ya kusamehewa kutokana na klabu kukabiliwa na mchezo muhimu, amedaiwa kueleza wazi kwamba sasa ameshachoshwa na `mizengwe` iliyoshika kasi zaidi katika uongozi wa sasa wa klabu yake.
Inaelezwa kuwa uamuzi wa uongozi kupenda kutumia rungu la kufungia wachezaji kwa kisingizio cha utovu wa nidhamu pindi mchezaji anapokuwa mstari wa mbele kulalamikia jambo f\'lani, ni miongoni mwa yale yanayomkatisha tamaa.
Akizungumza na Lete RAHA mwishoni mwa wiki, mmoja wa watu waliodai ni maswahiba wa Swedi amesema mkali huyo wa pembeni kulia mwa uwanja amevunjwa moyo na hali ya mambo klabuni kwao kwa sasa na huenda akaachana na klabu yake hiyo anayoipenda sana, labda baadhi ya viongozi wakumbuke wajibu wao klabuni na kuacha kuendeleza ubabe.
``Maslahi ni kitu muhimu... kama mchezaji anazinguliwa kulipwa jasho lake na bado akaamua kujitolea kwa mapenzi yake kwa klabu, anapaswa kuheshimiwa,`` amesema swahiba wa Swedi.
``Lakini hali haiko hivyo. Baadhi ya viongozi wanatanguliza ubabe badala ya kuwajali wachezaji. Zaidi wanaficha ukweli wa mambo kwa kuwasingizia wachezaji kuwa ni watovu wa nidhamu.
``Nadhani jambo hilo ndilo linaloelekea kumkatisha tamaa (Swedi),`` amesema swahiba huyo wa Swedi.
Na linaweza kumkatisha tamaa zaidi kwasababu mmoja wa watoa adhabu hizo za kufungia katibu mkuu wa Simba Mwina Kaduguda aliwahi kuondoka na mipira ya mazoezi ya timu kambini kutokana na kuzungushwa kulipwa shilingi 6,000 tu alizonunulia chapati za wachezaji mjini Morogoro wakati akiwa mkalimani wa kocha Mbrazili Naider Dos Santos mwaka 2006.
Kabla ya kikao cha uongozi kilichofanyika Alhamisi iliyopita, Swedi na wachezaji wengine watano wakiwemo Erick Majaliwa, Athumani Machupa, Victor Coasta, Yahaya Akilimali na Nurdin Bakari walisimamishwa klabuni kwao kwa madai ya kuwashawishi wenzao kufanya mgomo, hasa baada ya `kuzinguliwa` mishahara yao kwa miezi miwili.
Hata hivyo, wote waliotuhumiwa kwa makosa hayo wakasamehewa na taarifa zaidi zikasema kocha Mserbia Milovan Cirkovic anao uhuru wa kuwatumia leo dhidi ya Yanga, kama ataona kuwa wako fiti.
Hata hivyo, baadhi ya wachezaji hao akiwemo Athumani Machupa, wamedaiwa kujiweka kando na kukwepa kutia mguu kambini katika muda mfupi uliobaki kabla ya pambano lao la leo, wakihofia kuweza kuzuliwa `mizengwe` itakayowaharibia mustakabali wa ajira zao katika soka.
KIZINGITI
Ukiachana na sintofahamu inayoelekea kuiandama Simba hasa baada ya taarifa nyingine kuwa uongozi umemfungia pia mlinzi wa kati Henry Joseph, Swedi anaendelea kuwa mmoja wa wachezaji nyota ambao kukosekana kwao kunaweza kuleta unafuu kwa `fowadi` ya Yanga iliyopeleka ubingwa wa Bara jangwani kabla hata ya kumalizika kwa ligi.
Uwezo wake wa kuzuia na kupanda mfululizo kwa ajili ya kusaidia mashambulizi katika muda wote wa mchezo ni sababu mojawapo kati ya zile zinazompa heshima ya kuwa kizingiti muhimu katika safu ya ulinzi ya Simba.
Aidha, kashkash zake mbele ya lango la maadui ambazo mara kadhaa zimemlipa kutokana na mabao matamu aliyowahi kuyafunga katika misimu tofauti tangu ajiunge Simba miaka mitano iliyopita, ni baadhi ya sababu zinazoweza kuwakosesha mashabiki wa Simba `utamu` wanaoutarajia leo.
``Sidhani kama kaba yake ya akili na krosi zake bomba zitaweza kuonekana leo, katika mechi zilizobakia na hata msimu ujao ... amekatishwa tamaa na baadhi ya mambo yanavyoendeshwa klabuni,`` imeelezwa.
|