|
Mundu yapania ubingwa Zanzibar
2008-04-27 09:58:15
By Bahati Mollel
Timu ya Mundu imesema imepania kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya soka ya Zanzibar na ndiyo maana inaongoza msimamo baada ya kukamilika kwa mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 26.
Katibu mkuu wa Mundu Mussa Diku aliiambia Lete RAHA kwa njia ya simu juzi Ijumaa kuwa lengo lao sio kuongoza ligi hiyo bali ni kutwaa ubingwa ili kucheza kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwakani.
Diku alikisifu kikosi cha timu yake kuwa ni bora zaidi tofauti na cha miaka miwili iliyopita.
``Hii Mundu ya sasa ni tishio, sio sawa na ile ya mwaka juzi. Tunaamini tutaweza kutwaa ubingwa na kuiwakilisha nchi bila wasiwasi,`` alisema Diku.
Kama itatwaa ubingwa itakuwa mara ya kwanza kwa Mundu kucheza Ligi ya Klabu Bingwa lakini si michuano ya klabu ya Afrika.
Mwaka 2006 Mundu ilicheza Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika na kutolewa katika raundi ya kwanza na Highlanders ya Zimbabwe kwa jumla ya mabao 6-1.
Mundu imeshinda mechi nane na kutoka sare mbili kati ya michezo 11 ya duru la kwanza, ikifuatiwa na mabingwa watetezi Miembeni yenye pointi 25 kutokana na kushinda mechi saba na kutoka sare nne.
|