|
Mwaka wa Yanga
2008-04-27 10:02:13
By Mwandishi Wetu
Simba na Yanga zinakutana leo kwenye Uwanja wa Taifa katika moja ya mechi za kufunga msimu wa ligi kuu huku mabingwa wapya hao wa Bara wakiwa katika nafasi nzuri ya kumfunga mtani wake wa jadi kwa mara ya kwanza katika miaka nane.
Yanga ambayo iliivua Simba ubingwa wa Bara katika mchezo dhidi ya Prisons Jumapili iliyopita ilipofikisha pointi 48, haijaifunga Simba katika mchezo wa ligi kuu tangu ushindi maarufu wa 2-0 wa Agosti 5, 2000 ambapo mabao yote yalifungwa na Iddi `Bwana Harusi` Moshi.
Lakini leo Jumapili, miaka minane baadaye, Yanga ipo katika nafasi nzuri ya kubadili historia kutokana na kuwa katika mazingira mazuri kisaikolojia na kimchezo.
Kisaikolojia, Yanga si tu inarudi kwenye Uwanja wa Taifa kucheza mechi yake ya kwanza tangu itwae ubingwa wake wa 21 wa Bara lakini pia itakabidhiwa kombe mara baada ya mechi hiyo.
Ni wazi Yanga haitopenda kutia dosari sherehe hizo za kukabidhiwa kombe kwa kuendeleza uteja kwa Simba katika siku ambayo ushindi kwa Wekundu wa Msimbazi pia hauna maana zaidi ya kuendeleza historia ya miaka nane.
Lakini pia kimchezo wachezaji wa Yanga wataingia uwanjani wakiwa katika hali bora kiushindani kutokana na tofauti ya aina ya maandalizi ya kambi hizo mbili.
Ili kujiweka sawa kwa ajili ya mchezo muhimu wa leo, wachezaji wa Yanga, tena wengi wakiwa ni wa kikosi cha pili cha kocha Dusan Kondic, walikuwa na uwezo wa kutocheza kwa bidii na kupelekea kufungwa na Kagera Sugar mabao 3-1 Jumatano katika siku ambayo Simba ilitumia nguvu zote kutoka sare ya 2-2 na Polisi Dodoma.
Aidha, wakati Kondic atakuwa na tatizo la kujivunia la kuchagua timu ya kwanza kutoka kikosi kamili alichokuwa nacho tangu aanze kazi mwishoni mwa mwaka jana, Milan Cirkovic wa Simba atakosa wachezaji kadhaa waliofungiwa ama waliotoka kifungoni baada ya kulalamikia kutolipwa mishahara ya miezi mwili.
Henry Joseph amefungiwa wiki mbili na kuiachia Simba pengo kubwa katika safu ya kiungo-mlinzi lakini wachezaji kadhaa maarufu akiwemo beki Said Sued wamedai kutocheza leo wakipinga kudhalilishwa na uongozi wa Hasaan Dalali.
Aidha, wakati mishahara ya wachezaji ikiwa sitatizo Yanga, tatizo la malipo kwa wachezaji wa Simba lilitiwa makali na kukosekana kwa fedha za kuweka kambi makini kwa ajili ya pambano la leo.
Je kukosekana huko kwa utulivu katika kambi ya Simba na kuwepo kwa sababu, ari na uwezo wa timu ya Yanga kushinda hakutamaliza uteja leo?
Inawezekana Yanga isimalize uteja leo kama bahati uwanjani na rekodi ambavyo hutoa mchango mkubwa katika matokeo ya mchezo maridadi wa soka, vitaendelea kuiwakia Simba.
Timu zinatarajiwa kuwa:
Simba: Juma Kaseja, Salum Kanoni, Ramadhani Wasso, David Naftali, Kelvin Yondani, Mohammed Banka, Moses Odhiambo, Ramadhani Chombo, Mohammed Kijuso, Emmanuel Gabriel, Ulimboka Mwakingwe.
Yanga: Benjamin Haule, Fred Mbuna, Nadir Haroub `Canavaro`, Wisdom Ndlove, Hamis Yusuf, Abuu Ntiro, Mrisho Ngassa, Abdi Kassim, Ben Mwalala, Maurice Sunguti.
|