|
Daz Baba:Nunda anayerejea baada ya `kifo` cha Nundaz
2008-05-04 09:25:59
By Amour Hassan
Kufukuzwa kwa Daz Baba kundini Daz Nundaz mwaka 2006 pengine kulihitaji tafakari zaidi kabla ya maamuzi hayo kupitishwa.
Pengine juhudi za kutafuta muafaka wa matatizo yaliyojitokeza hadi kufukuzwa kwake, zingeweza kulinusuru kundi hilo lililotingisha vyema chati za muziki wa Bongofleva tangu lilipoibuka mwaka 1999 na single kali ya `Maji ya Shingo`, `Kamanda` hadi `Barua`.
Pengine Daz Nundaz ingeendelea kuwepo kwenye chati hivi leo ikichuana na makundi yaliyo katika chati ya Wanaume Family na Wanaume Halisi baada ya kusambaratika kwa makundi kibao katika mwaka wa shetani.
Lakini kwa maamuzi ya kumfukuza Daz Baba yaliyotolewa na memba wengine wa kundi hilo lililokuwa likiundwa na wasanii watano pamoja na kinara wao Ferooz, La Rhumba, Sajo a.k.a Chupa na Critic, Daz Nundaz ni kama imekufa.
Licha ya kiongozi wa memba waliosalia kundini Ferooz kusisitiza mara kadhaa kuwa kundi hilo bado lipo, Daz Nundaz haijaweza kuthibitisha kivitendo bado kama kweli iko hai.
Kilichodhihirika ni kuwa kuondoka kwa Daz Baba kundini ilikuwa kama nuksi kwa ustawi wa kundi hilo kwani mambo yote yalianza kwenda kombo.
Mpango uliokuwepo wa `kuwatoa` pamoja katika albam ya nje ya kundi memba watatu wa kundi hilo -- La Rhumba, Sajo na Critic - ulikufa muda mfupi baadaye baada ya La Rhumba naye kujitoa Daz Nundaz.
La Rhumba alijitoa huku memba hao watatu wakiwa tayari wameanza kurekodi nyimbo kwa ajili ya albam yao binafsi waliyopanga kuitoa chini ya jina la Manunda Watatu.
Single yao moja iliyoitwa `Ipo Fresh` kwa ajili ya albam yao hiyo tayari ilishaenda hewani huku nyimbo nyingine zikiandaliwa kuwashirikisha wakali kibao akiwemo Dully Sykes na memba wa familia ya Nundaz Scout Jentaz, ambao walisharekodi na Daz Nundaz katika baadhi ya kazi zao zilizotangulia.
Kila kitu kikaharibika na nahodha wa jahazi la Daz Nundaz Ferooz alipozungumza na safu hii mwanzoni mwa mwaka huu alikiri kuwa albam ya Manunda Watatu haipo tena ``kwasababu La Rhumba ameshajitoa, haiwezi tena kuwa na kama ilivyopangwa.``
Hata hivyo, Ferooz alisisitiza kuwa bado yuko pamoja na memba wawili waliosalia Sajo na Critic na kwamba watasikika pamoja ``hivi karibuni``.
Baadaye La Rhumba akaripotiwa kuungana na Daz Baba aliyekuwa akiitangaza albam yake binafsi ya `Elimu Dunia` katika ziara ya mikoa ya Tanzania.
TANZANIANO
Ni katika ziara hiyo ambapo Daz Baba alipata wazo la kuanzisha kundi lake.
Chini ya jina la Tanzaniano, kundi hilo jipya likaanzishwa likihusisha wasanii watatu - Baba, La Rhumba na memba mpya Ali Mbongo.
Wimbo wa kwanza wa kundi hilo tayari umeachiwa hewani baada ya Daz Baba kukamilisha harakati za kuusambaza katika vituo mbalimbali vya radio wiki hii.
Muimbaji huyo nyota ameiambia Lete RAHA juzi Ijumaa kuwa wimbo huo uitwao `Model wa Afrika` umerekodiwa katika studio za Sound Crafters na umewashirikisha memba wawili, bila ya La Rhumba.
Daz Baba alisema: ``Katika wimbo huu wa kwanza tumeimba mimi na Ali Mbongo, La Rhumba hajashiriki, lakini tuko pamoja.``
Nyota huyo aliongeza kuwa wimbo huo ni utangulizi kwa ajili ya albam ya kundi lao la Tanzaniano ambayo maandalizi yake yameanza taratibu.
Mbali na albam hiyo ya kundi, Daz amesema yeye bado yupo chini ya lebo ya Bongo Records ya prodyuza P-Funk `Majani` hivyo pia ataendelea kufanya kazi zake binafsi kama msanii wa kujitegemea.
``Niliona kuna haja ya kuwa na umoja kwasababu umoja ni nguvu ndio maana nikaanzisha kundi hili, lakini kazi zangu binafsi pia zitaendelea,`` alisema Daz.
Alisema, hatahivyo, kwasasa amewekeza nguvu katika albam ya kundi na kwamba kazi zake binafsi zitafuata kulingana na maelekezo ya kutoka kwenye lebo yake.
``Majani ameniambia kwa sasa anafanya kazi fulani kwa ajili ya kuwatoa watu, mimi niwe tayari wakati wowote.
Hivyo nawataka mashabiki wangu wafahamu kuwa ninarejea, lakini kwa sasa wasikilize kitu hicho kipya cha Tanzaniano kilichopo hewani,`` alisema.
DAZ MWALIMU
Daz Baba, ambaye jina lake la kuzaliwa ni David Nyika, amesema anajipanga ili arejee kufanya vizuri katika `gemu` ya kizazi kipya ama zaidi ya alivyofanya katika albam yake binafsi ya`Elimu Dunia`.
Mkali huyo ambaye pia hufahamika kwa jina la Daz Mwalimu, alitamba mfululizo kwa ngoma zake kali kwa ajili ya albam yake hiyo iliyoingia sokoni mwaka 2006 na kuthibitisha uwezo wake mkubwa kisanaa.
Wimbo wake wa kwanza binafsi wa `Wife`aliomshirikisha Ngwair ulibamba kisawa sawa kabla ya kufunika tena alipoachia `Namba 8,`akimshirikisha rapa Fid Q.
Single yake ya `Usiku Huu` aliowashirikisha Mr Blue, Sajo na Alicom haikubamba `ki-hivyo` lakini alirejea kisawa sawa katika chati wakati alipoachia ngoma yake nyingine ya ukweli zaidi ya `Nipe Tano` aliomshirikisha Ferooz, Sajo na memba wa kundi la Scout Jentaz.
Baada ya hapo? Kimya! Kisha?
``Ndio nimerejea hivyo, mashabiki wakae tayari kuna makubwa yanakuja,`` anasema Daz.
|