|
Uongozi wa riadha unasubiri nini madarakani?
2008-05-04 09:27:10
By Amour Hassan
Jumatatu wiki hii michuano ya 16 ya ubingwa wa riadha wa Afrika ilianza jijini Addis Ababa, Ethiopia, lakini bila ya timu ya Tanzania.
Baadaye, katikati ya wiki, taarifa zikatolewa kuwa timu ya taifa imeondoka lakini ikiwa na wachezaji wanne - wanaume wawili wa mbio za mita 5000 na wanawake wawili wa mbio ngumu za mita 10,000.
Badala ya zaidi ya wachezaji 10 waliokuwa kambini, njia ya mkato ikaonekana ni bora kwenda.
Michuano hiyo ya kila baada ya miaka miwili na ambayo mwaka huu ni muhimu zaidi kutokana na kuwa sehemu ya kutafutia viwango vya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya Agosti, ilikuwa muhimu mno kwa timu nzima ya taifa kushiriki kama ilivyokuwa michuano ya kimataifa ya Scotland mapema mwaka huu ambayo timu ya Tanzania pia haikushiriki. Kabisa.
Ndipo Lete RAHA tunapojiuliza viongozi wa shirikisho la riadha, RT, wanasubiri nini kuuacha uongozi wa mchezo huo kwenye mikono ya watu wengine kwa ajili ya kunusuru uwepo na maendeleo ya mchezo wenyewe?
Katika hali ya kawaida, Lete RAHA tunaamini, viongozi wa RT walipaswa kuona kuwa kuwepo kwao madarakani ni kikwazo cha maendeleo ya mchezo wanaoupenda zaidi.
Ni mchezo wanaoupenda zaidi hasa ikizingatiwa kuwa karibu wote ni wanariadha, baadhi maarufu, wa zamani.
Kuwepo kwao madarakani kunaelekea kuwa ni kikwazo cha maendeleo ya mchezo wanaoupenda zaidi kwasababu ingawa ni ukosefu wa fedha uliosababisha timu ya taifa ishindwe kwenda kwenye michuano ya ubingwa wa Afrika katika mwaka wa Olimpiki:
SABABU YA MSINGI ya kukosekana kwa fedha za kuipeleka timu ya taifa kwenye michuano ya ubingwa wa Afrika katika mwaka wa Olimpiki ni UDHAIFU wa viongozi wenyewe katika kuweka mikakati ya kuwezesha kupatikana kwa fedha za nauli hiyo.
Tulitaraji kiongozi yeyote muadilifu angepima mwenyewe uzito wa udhaifu uliojitokeza katika utendaji wake na madhara ya kasoro hiyo katika uhai wa mchezo na chombo anachokiongoza - RT.
Na hapa ndipo ambapo tulitaraji, Lete RAHA, kuona viongozi wa RT wakijiuzulu mmoja baada ya mwingine kwasababu ya kutokuwa na uwezo wa kukusanya hata nauli ya kwenda Ethiopia, nchi jirani na majirani zetu wa Kenya.
Lakini pia ukaribu wa Ethiopia unaongezwa na ukweli kuwa kambi ya timu ya taifa ilikuwa jijini Arusha ambako ni `pua na mdomo` na Nairobi ambako kungepunguza kwa kiasi kikubwa ukubwa wa nauli ya ndege ya kwenda Ethiopia.
Uungwana ni vitendo, Waswahili walisema. Si majibu mazuri. Si sababu nzuri. Si visingizio vizuri.
Baada ya kushindwa mfululizo kufanikisha majukumu yaliyo chini ya wajibu wa uongozi, viongozi wa RT wanasubiri nini kujiuzulu?
|