|
Simba yawabeza mabingwa Bara
2008-05-04 09:30:51
By Mwandishi Wetu
Klabu ya Simba imebeza mabingwa wapya wa ligi kuu ya soka ya Bara Yanga kwa kuchukua kombe hilo pale tu Wekundu wa Msimbazi wanapopokwa pointi mezani.
Katibu mkuu wa Simba Mwina Kaduguda alisema jijini kuwa mara zote watani wao walipochukua ubingwa kulitokana na kuzidiwa pointi chache ambazo Wekundu wa Msimbazi walipokwa kwa kufanya makosa madogo madogo kwenye mechi za ligi hiyo.
Akizungumza na Lete RAHA wiki hii Kaduguda alisema mwaka 2005 Yanga ilifaidika na kuathirika kwa Simba kulikotokana na kupokonywa pointi sita baada ya timu ya Mji Mpwapwa kujitoa.
Mwaka 2006, Kaduguda ambaye aliwahi kuondoka na vifaa vya mazoezi vya timu msimu huo kutokana na kuudai uongozi shilingi 6000 za chapati alizonunulia wachezaji akiwa mkalimani kambini, alisema Yanga ilifaidika na kunyang`anywa pointi tatu kwa Simba kulikotokana na kumchezesha mshambuliaji Mussa Hassan `Mgosi` aliyekuwa na kadi tatu za njano.
`Mgosi` alicheza mechi ya ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar na baada ya Simba kutwaa ubingwa wa ligi kuu ndogo mwaka jana, Yanga imevikwa tena taji mwaka huu baada ya kosa la kuchezeshwa kwa Juma Nyosso aliyekuwa amefungiwa katika mchezo dhidi Coastal Union ya Tanga.
``Hawa ndugu zetu ubingwa wao haunogi kwani mara zote wamekuwa wakisubiri sisi tuathirike kwa kunyang`anywa pointi,`` alisema.
|