|
Tinoco kuondoa `vijeba`
2008-05-04 09:32:56
By Mwandishi Wetu
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, Marcus Tinoco amesema atawaondoa wachezaji wote wenye umri mkubwa katika kikosi hicho kabla ya kushiriki kwenye mashindano ya Afrika Mashariki na Kati yatakayofanyika Burundi baadaye mwezi Juni.
Tinoco alisema jijini kuwa anasubiri vielelezo, vikiwemo vyeti vya kuzaliwa vya wachezaji 42 aliowaita kwenye kikosi cha awali.
``Mimi sina vielelezo vyovyote na wanaokusanya ni wasimamizi wa soka,`` alisema. ``Sasa baada ya kuletewa ndio nitavikagua na nitakapoona kweli ni wakubwa basi nitawaondoa mara moja kwenye timu yangu.``
Alisema atawachuja wachezaji 17 hivi karibuni na kubaki na 25 tayari kwa mashindano hayo.
Timu hiyo leo inatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki na kikosi cha timu ya Academy iliyopo chini ya uangalizi wa kampuni ya Kiliwoodi.
Timu hiyo inalalamikiwa kwa kuita wachezaji wengi wenye umri mkubwa waliocheza kwenye timu za ligi kuu kwa muda mrefu.
Baadhi ya wachezaji waliopo katika timu za ligi kuu ya Bara ambao pia vielelezo vyao bado kumfikia Tinoco ni Uhuru Seleman (Coastal Union), Adam Kingwande, Himil Tale, Saleh Tendega, Seif Milanzi (Ashanti United), Ramadhani Chombo, Deogratius Mushi, Davis Naftari (Simba), Sunday Bakari, Tchebo Seleman (Manyema Rangers) na Mrisho Ngassa (Yanga).
|