|
50 Cent kutumbuiza leo
2008-05-04 09:35:54
By Jimmy Charles
Mwanamuziki maarufu wa muziki wa rap kutoka nchini Marekani, Curtis James Jackson III, maarufu kama `50 Cent` sambamba na kundi lake G-Unit, wanatarajia kutua nchini leo saa nane mchana kwa ajili ya kufanya onyesho moja kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, usiku wa leo.
Akizungumza na waandishi wa habari , Meneja Masoko wa Tigo Kelvin Twissa, alisema kuwa 50 Cent na kundi lake wanakuja nchini kwa kazi moja ya kutoa burudani kwa mashabiki wa kundi hilo.
Alisema 50 Cent atapokelewa na vikundi mbalimbali vya ngoma za asili vya hapa nchini lengo likiwa ni kumuonyesha mwanamuziki huyo na kundi lake utamaduni wa mtanzania.
Twissa, alisema kuwa 50 Cent na kundi lake watatua nchini leo mapema, ambapo mara baada ya kutua watapata mapumziko mafupi na baadaye kuelekea ukumbini tayari kwa ajili ya kufanya onyesho hilo.
Alisema mara baada ya kumaliza kazi hiyo iliyomleta 50 Cent na kundi lake wataendelea ziara yao katika nchi mbalimbali duniani.
Aliongeza kuwa ujio wa msanii huyo utaendelea kufungua milango ya kulitangaza jina la Tanzania kimataifa katika nyanja ya muziki pamoja na kutoa nafasi kwa wanamuziki wa Tanzania kujifunza zaidi kutoka kwa wasanii wa kimataifa.
|