|
JK boyz waua
2008-05-04 09:36:46
By Mwandishi Wetu, Mwanza
Timu ya taifa, Taifa Stars, jana ilipiga hatua kubwa kucheza fainali ya Kanda ya Afrika Mashariki ya michuano ya awali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani baada ya kuifunga Uganda, The Cranes, mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba hapa Mwanza jana Jumamosi.
Shaaban Nditi alietokea benchi kuchukua nafasi ya nahodha wa Stars Henry Joseph ndiye aliyefunga bao muhimu la pili ambalo linaitaka Stars iepuke kufungwa si zaidi ya goli moja katika pambano la marudiano wiki mbili zijazo ili kusonga mbele.
Kama itafanikiwa kutumia vizuri ushindi muhimu huo dhidi ya Uganda jijini Kampala wiki mbili zijazo, Stars itacheza na mshindi kati ya Sudan na Rwanda kwa ajili ya nafasi moja ya kuingia fainali zitakazochezwa nchini Ivory Coast Februari mwakani.
Stars iliandika bao la kwanza katika dakika ya 12 lililofungwa na mkongwe Emmanuel Gabriel aliyepokea krosi ya chinichini ya chipukizi Mrisho Ngassa, na kuunganisha wavuni kwa shuti.
Stars ingeweza kupata mabao zaidi kama washambuliaji wake, akiwemo Ngassa aliyekuwa nyota wa mchezo kwa kuisumbua mara kwa mara ngome ya Cranes wangekuwa makini.
Stars iliingia hatua ya pili baada ya kuifunga Kenya kwa jumla ya magoli 2-1, na Uganda waliwatoa Eritrea kwa jumla ya magoli 5-3.
Kocha msaidizi wa Stars Ali Bushir aliipongeza timu yake kwa kucheza vizuri na kwa utulivu mkubwa, na ameahidi kucheza kwa taadhari kubwa watakapokwenda kwenye mechi ya marudiano ili waweze kushinda.
Naye kocha wa Uganda Lazlo Scabo ambaye ni raia wa Hungaria ameilaumu safu yake ya kiungo kwa kucheza hovyo, lakini amesema wana uwezo wa kushinda katika mchezo wa marudiano utakaofanyika baada ya wiki mbili.
Timu zilikuwa:
Stars: Farouk Ramadhani, Salum Sued, Nadir Haroub `Canavaro`, Fred Mbuna, Amir Maftaha, Geofrey Bonny, Henry Joseph (Shabaan Nditi dk.46), Uhuru Suleiman (Ulimboka Mwakingwe dk.46), Abdi Kassim `Babi`, Mrisho Ngassa na Emmanuel Gabriel (Jerson Tegete dk.75).
Uganda: Sam Kawalya, Saimon Masaba, Lawrence Ssegawa, Joseph Owino, Geremaya Sebuira (Johnson Bagole dk.49), Mussa Doka, Danny Wagaruka, Stephen Bengo (Anthony Bongole dk.72), Geofrey Sserunkuma (Ronald Muganda dk.56), Caesar Okuthi na Owen Kasula.
|