Sababu za kupiga marufuku ukataji miti Moshi zaelezwa

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, mkuu wa wilaya hiyo, Kippi Warioba, alisema uharibifu wa mazingira katika wilaya hiyo unasababishwa kwa kiasi kikubwa na watu waliokuwa wakifika kuomba vibali vya kukata miti kutokuwa wakweli kwani wamekuwa wakikata miti mingi na kwenda kuuza nchi jirani.

"Kusitishwa kwa vibali hivyo kutasaidia wataalamu wa mazingira kufika katika sehemu husika na kujionea kama kweli kibali alichoomba muhusika ni cha mti unaostahiki kukatwa, lakini pia baada ya wataalamu hao kujionea basi watatuletea mrejesho kama kweli mti huo unastahiki kuvunwa na watapaswa kuupiga picha ili nasi tujionee."

"Hadi sasa hatujatoa tamko la utolewaji vibali, hivyo kama kutatokea mtu kuhitaji kuvuna mti itampasa aandike barua, lakini pia tuna taarifa za kisayansi kuhusu kukauka kwa vyanzo vya maji ndiyo maana tumeamua kusitisha," alisema.