Jafo ashangazwa mwendokasi kuchelewa

22Oct 2017
Beatrice Shayo
Nipashe Jumapili
Jafo ashangazwa mwendokasi kuchelewa

SERIKALI  amemtaka Mtendaji Mkuu  wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Mhandisi Ronald Lwakatare, kukutana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa ajili ya kuruhusu taa kuongoza mabasi hayo badala ya trafiki kama ilivyo sasa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alitoa agizo hilo juzi jijini Dar e s Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mfumo wa mabasi yaendayo haraka.

Jafo ambaye alitembelea vituo vya Morocco na Kivukoni, alisema kitendo cha trafiki kuongoza magari katika barabara za mfumo huo, kinasababisha magari hayo kutofika kituoni kwa wakati.

Alisema  abiria wamekuwa wanalalamikia mabasi hayo kutofika vituoni kwa wakati kwa sababu yanaingiliwa na trafiki wanaoongoza katika taa kuwachelewesha.

Aidha, Jafo alisisitiza umuhimu wa kutumia taa za kuongozea magari barabarani ili mfumo wa mabasi yaendayo haraka ukidhi malengo yaliyokusudiwa.

“ Ni bora kuacha taa ziwake ili magari yasikae kwa muda mrefu kwenye taa kwa kuwa inaharibu maana ya mwendokasi,” alisema Jafo.

Pia alishangazwa na baadhi ya mabasi ya ‘express’ kutoka Kivukoni hadi Kimara kutochukua abiria katika vituo vingine.

’“Unakuta mabasi yanashusha abiria Kivukoni na kuna kundi la abiria wanaohitaji kwenda moja kwa moja Kimara, lakini hayachukui abiria. Jambo hili linapaswa kurekebishwa kwani linasababisha kero kwa abiria,” alisema.

Aidha, Jaffo alisema kitendo cha waendesha bodaboda kukatiza katika barabara za mabasi ya mwendokasi kinahatarisha usalama wao na abiria wanaotumia mfumo wa mabasi.

Pia Waziri Jafo aliagiza Dart kufuatilia mchakato wa upatikanaji wa kadi ili kutumiwa na wananchi.

Awamu ya kwanza ya Dart ilianza kufanya kazi kuanzia Mei 10, mwaka jana na kwa sasa zaidi ya abiria 200,000 wanatumia usafiri huo kwa siku.

Habari Kubwa