Lukuvi achukua shamba la Manji

Uamuzi huo ulitangazwa na waziri huyo alipokuwa akizungumza katika kikao cha pamoja cha viongozi mbalimbali wa serikali, dini na vyama wa wilaya ya Kigamboni jana.

Alisema shamba la Manji linalochukuliwa na serikali lina ukubwa wa ekari 714 wakati la Amadori lina ukubwa wa ekari 5,400. 

Alisema kufutwa kwa umiliki wa mashamba hayo,  kumetokana na wamiliki kushindwa kuyaendeleza na kuwanyima fursa wananchi kufanya shughili za maendeleo.

Eneo ambalo Manji amefutiwa umiliki wake, lipo Geza Ulole, Kigamboni na aliipa klabu ya Yanga, Septemba mwaka jana wajenge uwanja wa kisasa.

Hafla ya kukabidhi eneo hilo kwa wanajangwani ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, na maofisa wa chama na serikali ya Kigamboni. 

Aliyepokea eneo hilo kwa niaba ya klabu ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa klabu, Mama Fatma Karume aliyefuatana na Mjumbe mwingine wa Bodi hiyo, Dk. Jabir Katundu.