Nape ashtuka TV kuvamiwa

Ziara ya Nape inatokana na kile kilichoenea kwenye mitandao ya kijamii jana kuwa mmoja wa viongozi wa serikali alitinga kwenye kituo cha televisheni cha Clouds akiwa na askari polisi na kuwabughudhi baadhi ya watangazaji waliokuwamo studioni.

Wakati taarifa hizo zikiendelea kusambaa kwa kasi mitandaoni, Waziri Nape aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa leo atatembelea kwenye makao makuu ya kampuni hiyo.

"Kesho (leo) asubuhi kama Waziri mwenye dhamana na habari, nitatembelea Clouds Media kujua kilichotokea. Nawaomba sana wanahabari nchini kutulia kwa sasa," ujumbe huo ulisomeka kwenye akaunti ya Twitter ya Nape.

Na alipotafutwa na Nipashe kwa simu jana jioni kuzungumzia ujumbe huo, Nape alikiri ujumbe huo ameuandika mwenyewe na leo atafanya ziara kwenye kampuni hiyo.

"Ni kweli, huo ni ujumbe wangu na kesho (leo) nitatembelea kituo hicho cha habari," alisema Nape.