Majeruhi yamuondoa Ulimwengu Stars

Stars inatarajia kuikaribisha Botswana Machi 25 na baadaye kuivaa Burundi Machi 28 mwaka huu, mechi zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini, Mkuu wa Idara ya Habari za Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema kuwa wamepokea taarifa kuwa Ulimwengu ni mgonjwa na sasa yuko chini ya uangalizi wa madaktari wa timu hiyo.

"Tunasikitika Ulimwengu hatakuja ila Samatta (Mbwana) yeye atakuja kama ilivyotarajiwa," alisema afisa huyo.

Aliongeza kuwa kikosi cha timu hiyo kilichoko chini ya Kocha Mkuu Salum Mayanga kinatarajia kuanza mazoezi leo kwa ajili ya kujiandaa na mechi mbili za kirafiki za kimataifa zitakazofanyika hivi karibuni, imeelezwa.

Wachezaji wengine walioko katika kikosi cha Mayanga ni pamoja na makipa; Aishi Manula (Azam), Said Mohamed (Mtibwa Sugar) na Deogratius 'Dida' Munishi (Yanga) huku mabeki ni Shomari Kapombe (Azam), Hassan Kessy (Yanga), Mohammed 'Tshabalala' Hussein (Simba), Gabriel Michael (Azam), Andrew Vincent (Yanga), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba) na Erasto Nyoni (Azam).

Viungo; Himidi Mao (Azam), Jonas Mkude (Simba), Salum 'Sure Boy' Abubakar (Azam), Said Ndemla (Simba), Frank Domayo (Azam), Muzamil Yassin (Simba), Simon Msuva (Yanga), Shiza Kichuya (Simba), Farid Mussa (DC Tennerife) na Hassan Kabunda (Mwadui FC).

Wengine ni pamoja na nahodha Samatta (K.R.C. Genk, Ubelgiji), Ibrahim Ajib (Simba), Mbarak Yussuf (Kagera Sugar) na Abdulrahman Mussa (Ruvu Shooting).