Mbegu za mbuzi wa asili hatarini kutoweka

27May 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Mbegu za mbuzi wa asili hatarini kutoweka

WAFUGAJI nchini wapo hatarini kupoteza mbegu za mbuzi wa kienyeji, baada ya wengi kuhamia kwenye ufugaji wa kisasa na kuacha ufugaji wa asili.

Hayo yalisemwa jana na Mratibu Mkuu wa mradi wa kuboresha, kuhifadhi na kuendeleza mbuzi wa asili, ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa mifugo Tanzania, kituo cha Tanga, Dk. Zabron Nziku, wakati akizungumza na kikundi cha wafugaji wa mbuzi weupe wa Kipare, waliotembelea kituo cha utafiti wa mifugo (TALIRI) kilichopo West Kilimanjaro kujionea shughuli za ufugaji.

Dk. Nziku alisema utafiti uliofanywa na watafiti wa mifugo wamebaini kuwapo kwa upotevu wa mbuzi wa asili ya kienyeji, kutokana na wafugaji wengi kuhamia kwenye ufugaji wa kisasa na kusahau wa asili.

Alisema lengo la mradi huo wa mwaka mmoja ni kutoa elimu na kuhamasisha ufugaji huo wa mbuzi weupe wa Kipare, ambao wana uwezo wa kuishi mazingira yote, huku wakistahimili ukame na hata magonjwa tofauti na mbuzi wengine wa kisasa.

"Ukifuga mbuzi hawa wa asili hutaingia gharama kubwa kama mfugaji au kama wale wanaofuga mbuzi wa kisasa," alisema.

Dk. Nziku alisema tangu kuanza kwa mradi huo, Januari mwaka huu zaidi ya wafugaji 100 wa mbuzi wamenufaika na mafunzo ya mbinu bora za ufugaji wa mbuzi hao weupe wa asili na namna ya kuhifadhi mbegu bora.

Aliushukuru Umoja wa nchi za Afrika na Umoja wa nchi za Ulaya kwa ufadhili, pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kukubali mradi huo kufanyika nchini.

Mkurugenzi wa Kituo cha utafiti wa mifugo (TALIRI) West Kilimanjaro, Dk. Athumani Nguluma, alisema kutokana na hali hiyo wafugaji wa mbuzi, wameshauriwa kutumia ufugaji wa mbuzi wa asili, ambao wapo hatarini kutoweka ili kurejesha asili iliyokuwapo hapo awali.

Aliwashauri pia kuwa na utaratibu wa kuchagua madume na majike ya mbegu yaliyo bora, wakati wa kupandisha mifugo ili vizazi vijavyo viwe bora zaidi.

"Sisi kama kituo tunahamasisha na kutoa elimu kwa wafugaji wetu wa mbuzi, kurudi katika kufuga mbuzi weupe wa asili ya kipare ili wasipotee, mradi huu umeanzia Wilaya ya Same na baadaye tutaenda wilaya zingine katika kuhakikisha tunahamasisha wafugaji wetu wanafuga mbuzi wa asili, ambao wana manufaa makubwa," alisema Dk. Nguluma.

Mmoja wa wafugaji wa mbuzi walionufaika na mradi huo, Athuman Hamahama, alisema kupitia mradi huo, wameweza kurudi kwenye ufugaji wa mbuzi weupe wa asili, ambao hapo awali walikuwa wakifuga mbuzi wa kisasa na kuingia hasara, tofauti na sasa wanapata manufaa makubwa kutokana na mbuzi hao kuwa na uwezo wa kustahimili magonjwa na mazingira yote magumu.