Mpango kuendeleza mazao kilimo waanza

14Oct 2020
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Mpango kuendeleza mazao kilimo waanza

SERIKALI imezindua mpango wa kuendeleza viwanda vya mazao ya kilimo utakaochochea uchumi wa viwanda hapa nchini na kuwanufaisha wakulima.

Mpango huo umeandaliwa na Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Afrika (AGRA) ili kusaidia kuinua sekta ya kilimo.

Akizungumza jana kwenye uzinduzi huo, Katibu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe, alisema mpango huo umelenga kutafuta fedha kwa ajili ya kusaidia viwanda hivyo ili Tanzania iendelee kupiga hatua zaidi kiuchumi.

"Tunashukuru AGRA kwa kuandika andiko la mpango huu ambalo tunaamini litakuwa na tija katika uchumi wa nchi yetu,” alisema Prof. Shemdoe.

Aidha, Prof. Shemdoe alisema kuwa andiko hilo litasimamiwa kupitia programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II).

Alisema mpango huo unatarajiwa kuleta matokeo chanya na kuongeza faida katika sekta ya kilimo nchini.

“Tunatakiwa kuendelea kukaa katika nchi zenye uchumi wa kati kwa kujenga viwanda vitakavyosaidia kuongeza ajira kwa vijana wanaohitimu kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini,” alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, alisema kuwa kupitia mpango huo serikali inatarajia kufanya mapinduzi ya viwanda ili kuwa na tija nchini.

Kusaya alisema kuwa mpango huo ukitekelezwa tatizo la ajira hapa nchini litakuwa historia kwa kuwa viwanda vingi vikijengwa vitasaidia kuondoa tatizo hilo.

Aidha, Kusaya alisema tayari Wizara ya Kilimo imeshaanza kufufua Viwanda vya Kilimo katika Mkoa Geita na Wilaya ya Chato ambavyo vilikuwa vikichakata pamba.

"Wizara itaendelea kuzindua hata viwanda vilivyosinzia lengo ni kuwa na viwanda vingi hapa nchini," alisema Kusaya.

Alisema serikali inaendelea kukuza sekta ya kilimo kwa kuzalisha mbegu bora, kutumia teknolojia za kisasa pamoja na kuongeza maofisa ugavi ambao watakuwa wakiwasaidia wakulima kulima kilimo chenye tija.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel, alisema mpango huo ni muhimu kwa taifa kwa kuwa lengo la Tanzania kufikia uchumi wa juu.

Top Stories