Mwanjelwa akunwa utendaji NFRA

03Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Mwanjelwa akunwa utendaji NFRA

NAIBU Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mary Mwanjelwa, amepongeza juhudi za  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa utendaji kazi kwa ubunifu kwa kuanzisha mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi mazao.

NAIBU Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mary Mwanjelwa.

Mradi huo utahusisha ujenzi wa vihenge vya kisasa, maghala ya kisasa na ukarabati wa ofisi na baada ya mradi huo kukamilika, wakala itakuwa imeongeza uwezo wa kuhifadhi tani 250,000 za mahini. 

Mradi huo unataraji kutekelezwa na kampuni mbili za ujenzi  kutoka serikali ya Poland za Feerum na Unia Arab kwa usimamizi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa gharama za Sh. bilioni 150.

Tayari maandalizi ya awali yameshakamilika ikiwamo utiwaji saini mikataba, uchunguzi wa udongo, tathmini ya athari ya mazingira na kutembelea eneo la mpango kazi.

Akizungumza wakati akikagua ghala la kuhifadhia mahindi la Kanda ya Makambako mkoani Njombe, Mwanjelwa alisema NFRA imefanya kazi kubwa ya ubunifu na kujiongeza kwa ajili ya kuwanufaisha wakulima katika kanda zote saba za Makambako, Kipawa (Dar es Salaam), Dodoma, Shinyanga, Arusha, Songea na Sumbawanga.

Alisema pamoja na Kanda ya Makambako kupangiwa kununua tani 6,500 katika msimu wa mwaka 2017/2018 na  baada ya lengo kukamilika, ziliongezwa fedha za ununuzi hivyo kununua tani 8,961.5 

Awali, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Vumilia  Zikankuba, alisema Makambako ni miongoni kwa kanda zitakazoongezewa uwezo wa kuhifadhi nafaka na tayari kuna kiwanja chenye ukubwa wa ekari 2,9965 kilichoko Makambako na kingine Mbozi chenye ukubwa wa  ekari 53.691.

Alisema NFRA imefanikiwa kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kununua baadhi ya mazao ya chakula cha ziada kutoka kwa wakulima, kutoa chakula cha ziada kwa waathirika, kutekeleza mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa  kutoa bei nzuri kwa wakulima wanaouza mazao yao kwa NFRA sambamba na utekelezaji wa malengo ya millennia. 

Top Stories