ACT yabainisha shida nane elimu

12May 2022
Halfani Chusi
DAR ES SALAAM
Nipashe
ACT yabainisha shida nane elimu

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeainisha vikwazo vinane vinavyoikabili sekta ya elimu nchini, hivyo kusababisha kuwapo mijadala mingi kuhusu sekta hiyo.

Msemaji wa Sekta ya Elimu wa ACT-Wazalendo, Riziki Shahari Mngwali jana mkoani Dar es Salaam, alibainisha vikwazo hivyo jana alipozungumza na waandishi wa habari, akisisitiza vinadidimiza ukuaji wa elimu nchini.

Alisema kutokana na umuhimu wa elimu, bajeti ya sekta ya elimu imekuwa ikifuatiliwa na wananchi na wadau mbalimbali, wakiomba vipengele kadhaa kufanyiwa marekebisho.

“Kwa hiyo niseme tu kuna maeneo manane ambayo ACT-Wazalendo imeona kama serikali isipoyafumbia macho, basi tutakuwa tumeboresha elimu yetu kwa kiasi kikubwa.

"Mambo yenyewe; Usimamizi duni wa utoaji wa elimu ya awali, msingi na shule za upili nchini; wanafunzi kukatisha masomo kabla ya kumaliza elimu ya msingi; udhibiti na ubora katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi hayapewi kipaumbele nchini.

"Hakuna elimu bila walimu, serikali imalize tatizo la uhaba wa walimu; Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inaendeleza ubaguzi katika mfumo wetu wa elimu; mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya miradi ya maendeleo ya elimu; haki ya elimu kwa mtoto wa kike; pamoja na elimu ya mafunzo ya vitendo kwa elimu ya juu."

Riziki pia aliikosoa serikali kwa kusuasua kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Elimumsingi Bila Malipo, maarufu elimu bure, pia alichokiita ulegevu katika utoaji huduma za elimu na ujenzi wa miundombinu ya elimu.

“Mwaka 2016 serikali ilianza kutekeleza mpango wa elimumsingi bila malipo, huu ni mkakati mzuri wa serikali kuhakikisha watoto wote wa Kitanzania wanapata elimu ya msingi bila kikwazo cha ada.

"Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kuna upungufu mkubwa sana wa walimu kuanzia ngazi ya awali, shule za msingi na upili, pia kuna upungufu wa vyumba vya madarasa na vitabu, hivyo kwa muda mrefu serikali imeshindwa kufanya ukaguzi wa ufanisi kwenye shule za msingi na upili ili kukagua na kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa," alifafanua.

Aliishauri serikali kuhakikisha kila mtoto wa kike aliyepata mimba akiwa shuleni, anamaliza elimu yake kama ilivyokusudiwa kwa kusimamia ahadi ya kuruhusu kumrejesha mtoto wa kike shuleni.