Aliyebaka na kumuua mke wa Mwenyekiti akamatwa

21Feb 2023
Na Mwandishi Wetu
Bukoba
Nipashe
Aliyebaka na kumuua mke wa Mwenyekiti akamatwa

JESHI la Polisi mkoani Kagera limemkamata kijana Paschal Kaigwa (22) mzaliwa wa Kishogo Bukoba Vijijini, ambaye anatuhumiwa kumbaka na kumuua mke wa Mwenyekiti wa Mtaa wa National Housing kata ya Rwamishenye katika manispaa ya Bukoba, Khadija Ismail (29).

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera William Mwampaghale amesema kuwa mtuhumiwa huyo alijificha katika vichaka na kwamba baada ya kukaa huko bila chakula, aliamua kutoka mafichoni na kwenda nyumbani kwa shangazi yake katika mtaa wa Katatorwansi ulioko katika manispaa ya Bukoba.

Imeelezwa kuwa alipofika alikuta watoto ambao baada ya kumuona walipiga kelele na kuwezesha wananchi kumkamata.

"Njaa ilimtoa mafichoni akaenda kwa shangazi yake, lakini watoto aliowakuta pale walikuwa tayari wana taarifa, kutokana na taarifa zenu mlizozitangaza kuwa anatafutwa, tumemkamata juzi tarehe 19/02/2023 saa kumi jioni, tunaye, tunamhoji na tutamfikisha kwenye vyombo vya kishera" amesema Kamanda huyo.

Februari 13 mwaka huu majira ya jioni, kijana huyo ambaye alikuwa amepewa hifadhi nyumbani kwa mwenyekiti wa mtaa huo kutokana na kutokuwa na mahali pa kuishi, anadaiwa kumbaka na kumuua mke wa mwenyekiti na kisha kutoweka.

Top Stories