Jaji Mkuu mstaafu Chande aagwa akimiminiwa sifa

03Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Jaji Mkuu mstaafu Chande aagwa akimiminiwa sifa

JAJI Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, ameagwa rasmi kimahakama, baada ya kustaafu utumishi wa umma.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi (kulia), akiagana na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, baada ya hafla fupi ya kumuaga, iliyofanyika katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam jana. PICHA: MIRAJI MSALA

Alistaafu baada ya kuwa Jaji Mkuu kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi mwaka 2017, na aliagwa katika sherehe iliyofanyika jana katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

Jaji Othman Chande aliushukuru uongozi wa serikali kuanzia awamu ya tatu chini ya Benjamin Mkapa kwa kumpa dhamana ya kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, pamoja na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, na hatimaye Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli kwa kuendelea kumwamini na kufanya nao kazi hadi alipostaafu mwaka juzi.

Jaji Chande alisema Mahakama ya Tanzania inazingatia mgawanyo wa madaraka katika utendaji kazi wake, na kuyafanyia kazi maoni ya umma pale yanapokusanywa ili kuboresha na kuimarisha huduma za kimahakama ili hatimaye ziweze kuwafikia wananchi kwa wakati.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma, alimweleza Jaji Othman kuwa, serikali inatambua umuhimu wake na kazi zake alizofanya zimekuwa chachu ya maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika katika Mahakama ya Tanzania.

“Serikali inatambua umuhimu na mchango wako katika kuimarisha maboresho ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi katika Mahakama ya Tanzania, pia tutaendelea kuufanyia kazi ushauri wako ambao unaendelea kutupatia kama Jaji mkuu mstaafu,” alisema Prof. Juma.

Nao baadhi ya majaji waliohudhuria katika hafla hiyo, walimwelezea Jaji Mkuu mstaafu Chande kuwa ni mtu mwenye weledi na anayesimamia sheria za Mahakama, na ametoa mchango mkubwa katika maboresho yanayoendelea katika Mahakama na wataendelea kumuenzi kwa vitendo kwa kutumia busara zake na hekima aliyonayo katika kazi zao za kila siku.

Jaji Mkuu mstaafu Chande alizaliwa Januari Mosi, 1952, ana Shahada ya kwanza ya Sheria (LLB) ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam na Shahada ya Uzamili (MA) kutoka Chuo Kikuu cha Webster Geneva, Uswisi.

Aliwahi kuwa Makamu wa Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Rwanda (ICTR) jijini Arusha na amewahi kushika nafasi sawa na ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nchini.

Kadhalika, Jaji Chande amewahi kufanya kazi ndani na nje ya nchi katika mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kama vile Shirika la Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na Shirika la Msalaba Mwekundu. Pia ni mtaalamu mbobezi katika masuala ya Sheria za Haki za Binadamu.