Mfanyabiashara adaiwa kutekwa

02Jul 2019
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Mfanyabiashara adaiwa kutekwa

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameitaka serikali kuchukua hatua kuhusu kutoonekana kwa mfanyabiashara Raphael Ongangi, anayedaiwa kupotea kwa wiki moja sasa.

Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe, akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kuhusu kutekwa kwa aliyekuwa msaidizi wake, Raphael Ogangi, na kuiomba serikali kulichukulia uzito jambo hili ili kuweza kumpata kwa haraka. PICHA: GETRUDE MPEZYA

Jeshi la Polisi limekiri kupokea taarifa za madai ya kutekwa kwa mfanyabiashara huyo na linaendelea kuzifanyia kazi.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Zitto alidai mfanyabiashara huyo ambaye ni raia wa Kenya, amekuwa nchini tangu mwaka 2002 na aliwahi kuwa msaidizi wake.

"Raphael alikuja hapa nchini tangu mwaka 2002 na alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea shahada ya biashara, na akiwa nchini, alipata marafiki wengi wa Tanzania na hata kufunga ndoa na Mtanzania," alisema.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, alidai mfanyabiashara huyo alitekwa maeneo ya Osterbay jijini akiwa na mke wake, Veronica wakitokea shuleni kwa mtoto wao kulikokuwa na kikao cha wazazi.

Alidai kulitokea gari  lililowazuia kwa mbele na waliokuwamo kuwatolea silaha aina ya bastola na kuwachukua wote wawili na baadaye mkewe aliachiwa, huku Raphael wakiondoka naye.

Zitto alidai tangu kutekwa kwa mfanyabiashara huyo Jumatatu Juni 24, mwaka  huu, tayari ameshalifikisha suala hilo katika mamlaka mbalimbali za likiwamo Jeshi la Polisi alikoripoti kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Alidai ameripoti kwenye idara nyingi za serikali zinazohusu uchunguzi wa masuala nyeti na kutoa taarifa muhimu zikiwamo namba za magari yaliyotumika kumteka Raphael, lakini hawajafanikiwa kupata taarifa kutoka kwenye idara hizo kuhusu mfanyabiashara huyo.

Hata hivyo, Zitto alidai marafiki wa mfanyabiashara huyo wamefanikiwa kupata taarifa muhimu kuhusu magari yaliyotumika kumteka na alikowekwa mfanyabiashara huyo. 

"Sisi marafiki wa Raphael kwa kutumia msaada wa marafiki zetu nje ya nchi, tumefanikiwa kupata alipowekwa Raphael baada ya kutekwa, pia tumefanikiwa kupata namba za magari yaliyomteka Raphael," Zitto alidai.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo aliiomba Serikali ya Kenya kufuatilia suala hilo, akiahidi kutoa ushirikiano kwayo kwa kuikabidhi taarifa walizofanikiwa kuzipata kuhusu mfanyabiashara huyo.

"Sisi tunaikabidhi Serikali ya Kenya ushahidi kwa kila mahali alipokuwa Raphael tangu siku ametekwa mpaka sasa," Zitto alisema.

KAULI YA POLISI

Alipoulizwa na Nipashe jana mchana kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema suala hilo ni dogo na ameshamruhusu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Konondoni kulizungumzia.

"Hili suala ni dogo, nimeshamruhusu Kamanda wa Polisi Kinondoni alizungumzie tangu mwanzo, mtafute yeye umuulize," Mambosasa alisema.

Alipotafutwa na Nipashe kulizungumzia, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Musa Taibu, alikiri jeshi hilo kupokea taarifa kutoka kwa Zitto aliyelieleza kuhusu alikohisi Ongangi amefichwa.

"Taarifa hizi alizileta Jumamosi na askari wangu waliondoka na Zitto hadi kwenye eneo ambalo alidai anahisi Ongangi ametekwa, baada polisi kufika walifanya ukaguzi maeneo hayo lakini hawakumkuta," Kamanda Taibu alidai.

Kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi alidai kuwa hadi sasa, jeshi hilo halijathibitisha kama taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo ni za kweli ama la kwa kuwa limezipokea kutoka kwa Zitto.

Hata hivyo, Kamanda Taibu alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Oktoba 11, mwaka jana saa 11 alfajiri, mfanyabiashara maarufu, Mohamed Dewji 'Mo', alitekwa na watu wasiojulikana kwenye Hoteli ya Colosseum iliyoko Oysterbay jijini alikokwenda kufanya mazoezi kwenye gym ya hoteli hiyo kisha kuachiwa usiku wa kuamkia Oktoba 20.

Baada ya kupatikana kwa Mo ikiwa ni siku tisa tangu kutekwa kwake, Jeshi la Polisi lilieleza kuwa alipatikana akiwa ametelekezwa ndani ya gari eneo la Viwanja vya Gymkhan jijini.

Imeandikwa na Enock Charles na Romana Mallya