Mshtuko Mbunge aliyefariki ghafla

12Nov 2016
Augusta Njoji
Nipashe
Mshtuko Mbunge aliyefariki ghafla

Tahiri ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma, alikuwa miongoni mwa Wabunge walioteuliwa kusafiri kwenda Urambo mkoani Tabora ili akamzike Spika Mstaafu wa Bunge, Samuel Sitta, leo.

Samuel Sitta

Alijitabiria kifo
Novemba Mosi, mwaka huu, Tahir aliuliza swali bungeni, akihoji kwa nini serikali haioni umuhimu wa kuweka utaratibu utakaofanya, Mbunge wa jimbo akifariki dunia, aliyekuwa akimfuata kwenye mchuano wa kutafuta mgombea ndani ya chama, ashike nafasi iliyo wazi badala ya uchaguzi kurudiwa.

Alihoji pia kwa nini serikali haioni ni wakati muafaka kuondoa utaratibu wa kusimamisha uchaguzi mkuu, mgombea mmojawapo anapofariki dunia.
Alisema uchaguzi wa marudio unasababisha upotevu wa fedha, jambo linaloweza kuepukika kwa faida ya Watanzania.

Akijibu swali hilo la Tahir, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Walemavu, Dk. Abdallah Possi, alisema sheria ya uchaguzi na mfumo wa uchaguzi uliopo, unamwelekeza mpigakura kumpigia mtu na si chama kama ilivyo kwenye mifumo mingine ya kupigia kura chama.

Alisema mpango anaoutaka Tahir, unaweza kuwa mzuri ikiwa utapitia hatua zote za marekebisho ya sheria mpaka ufike Bungeni.

Alisema kwa sasa serikali itaendelea kutumia utaratibu uliopo kwa sababu mshindi wa pili atakayechukuliwa kujaza nafasi wazi, atakuwa hajachaguliwa na wananchi wote nchini au jimboni au kata bali wanachama wachache wa chama hicho.

Alikwenda hospitali mwenyewe
akafariki dakika 15 baadaye
Akizungumzia kifo cha Mbunge huyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Caroline Damian, alisema Tahir alifika kwenye hospitali hiyo peke yake saa 7:50 usiku akisumbuliwa na shinikizo la damu.

Alisema baada ya kufika alianza kupatiwa matibabu ya awali, lakini baadaye hali yake ilibadilika na kupelekwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) na kufariki dunia saa 8:05 usiku.

“Alikuwa amepatiwa matibabu ya awali kule Bima ya Afya baadaye walimkimbiza ICU hali yake ilipobadilika ghafla kwa sababu alikuja mwenyewe. Yaani kifo chake kimetokea ndani ya dakika 15 baada ya kufika hospitalini,” alisema Dk. Damian.

Mganga huyo alisema mbunge huyo alipofika hospitalini hapo alikuwa anajitambua na kwamba aliweza kujieleza vizuri tu.
Tahir amefariki siku moja baada ya kuchaguliwa kuwa Katibu wa Tawi la Wabunge wa Yanga.
Wabunge wamzunguzia

Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, alisema: "Ametutoka ghafla, leo (jana) alipangwa kwenda kumzika Sitta huko Urambo.”
Naye Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, alisema: “Jana (juzi) tulikuwa naye kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji ya Bunge Sports Club hadi saa tatu usiku na alichangia vizuri tu bila kuonyesha udhaifu wowote wa kiafya. Bwana alitoa na sasa ametwaa, jina lake lihidimiwe.”.

Mwili wa Mbunge huyo uliwasili katika viwanja vya bunge saa 3:30 asubuhi ukitokea Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma ulikokuwa umehifadhiwa na uliwekwa kwenye lango la kuingia wabunge na kutoa nafasi kwa wabunge kutoa heshima za mwisho ukiwa umefunikwa bendera ya bunge.

Viongozi walioongoza wabunge kutoa heshima za mwisho ni Spika wa Bunge Job Ndugai, Naibu Spika Dk. Tulia Ackson, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freemon Mbowe.

Wakitoa salamu za rambirambi, Ndugai alisema amestushwa na taarifa za kifo cha mbunge huyo kwa kuwa juzi kabla ya kukumbwa na mauti, alishiriki kikao cha Timu ya Wabunge New Dodoma Hotel kupanga mipango ya kwenda kushiriki mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki.
Alisema pia marehemu alikuwa mmoja wa wabunge ambao waliomba kwenda kwenye mazishi ya Spika Mstaafu wa Bunge. Alisema kikao hicho kilikuwa kizuri na baada ya kumaliza

Wabunge wasamehe posho
Ndugai alisema kutokana na msiba wa mbunge huyo pamoja na ule wa Sitta, posho za wabunge za kikao cha jana zitagawanywa nusu kwa nusu kwa misiba hiyo.

Waziri Mkuu, Majaliwa, kwa upande wake alisema: “Leo (jana) tunazungumza akiwa katika hali nyingine ni jambo la huzuni kwetu na ni funzo kwetu pia. Serikali kupitia Rais Dk. John Magufuli inatoa salamu za pole sana kwa Spika wafiwa wote, leo wabunge tupo kwenye hali ngumu tumepoteza wabunge wenzetu ambao tulikuwa nao kwenye bunge,” alisema Majaliwa.

Naye Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freemon Mbowe, alisema msiba huo uwe somo kwa wabunge kwa kuwakumbusha kupendana na kuheshimiana huku akisema Hafidh alikuwa mcheshi na mstaarabu.

“Safari ya Tahir ni yetu sote, katika maisha haya tumepewa na Mwenyezi Mungu na ana mamlaka ya kuchukua wakati wote ni vyema tukaishi na kutambua tofauti zetu hapa duniani ni za muda mfupi. Alikuwa mwana Yanga mwenzangu, alikuwa mtu wa kuunganisha wabunge pamoja na tofauti za kisiasa hajawahi kukwazana na mbunge,” alisema Mbowe.

Alisema misiba iliyowakumba wabunge inawakumbusha kupendana, kuheshimiana kwa kuwa Mwenyezi Mungu anaweka ushuhuda kwenye macho yao.
Mwakilishi wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Almas Maige, alisema atakumbukwa katika uamuzi wa kamati hiyo kwa kusimamia ukweli wakati wote.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, alisema Tahir alikuwa mjumbe wa kamati hiyo na walikuwa naye tangu juzi, kamati hiyo imepata pigo kubwa sana.

“Mheshimiwa Tahir alikuwa mcheshi, alipenda kutuchekesha pale tunapokuwa tumechoka. Pale tulipokuwa tukifanya kazi hadi usiku, alikuwa mchangiaji mzuri sana, wakati mwingine Kiswahili cha Kisukuma au Kipare alitusahihisha. Tarehe 26, mwezi huu, alitualika kwenda Zanzibar akifungua michezo,” alisema Mwenyekiti huyo.

Ndani ya Bunge
Wabunge walisimama kwa dakika moja kumuombea huku Ndugai akisema kwa mujibu wa kanuni ya Bunge 152 ambayo inasema inapotokea mbunge atafariki dunia wakati wa Bunge likiwa katika shughuli zake, Spika ataahirisha shughuli za Bunge kwa siku hiyo kwa ajili ya maombolezo.

Hata hivyo, Ndugai alisema kutokana na bunge kuwa na kikao maalum kwa ajili ya kumuaga Marehemu Sitta, aliomba kutenguliwa kwa kanuni hiyo ili shughuli za bunge zisitishwe kwa muda na kuendelea na kikao hicho.

Ndugai alimtaka Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, kutengua kanuni hiyo ili shughuli za jana zifanyike.

Shughuli nyingine ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo, Andrew Chenge, kuhitimisha hoja yake ya taarifa ya utendaji kazi ya kamati iliyowasilishwa juzi ili ikafanyiwe kazi na serikali bila kuwepo na mjadala.

Baada ya kutengua kanuni hiyo, Chenge aliruhusiwa kuhitimisha kwa muda mfupi hoja yake bila kuchangiwa na wabunge tofauti na utaratibu mwingine unaofanyika bungeni

Top Stories