Panga lawafyeka vigogo kibao balozi za Tanzania

26Jun 2016
Joseph Mwendapole
Nipashe Jumapili
Panga lawafyeka vigogo kibao balozi za Tanzania

KUNA taarifa kuwa panga kali linatembea la kuwapunguza vigogo mbalimbali katika ofisi za balozi za Tanzania zilizoko ughaibuni ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kubana matumizi yasiyo ya lazima.

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Augustine Mahiga

Hali hiyo itawezesha fedha zinazookolewa zielekezwe katika miradi ya maendeleo inayowagusa moja kwa moja wananchi wa kawaida.

Hadi sasa, tayari vigogo kadhaa wa ofisi hizo za balozi za Tanzania kwenye nchi mbalimbali duniani wameshakumbwa na hatua hiyo inayotekelezwa kwa umakini mkubwa na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

Hivi karibuni, Wizara hiyo ilitoa taarifa iliyothibitisha kuwapo kwa mpango wa kuwapunguza maafisa na watumishi wengine mbalimbali kwenye ofisi za ubalozi baada ya kubainika kuwapo kwa idadi kubwa ya watumishi isiyoendana na mahitaji halisi ya kazi zilizopo.

Akizungumza na Nipashe hivi karibuni, waziri katika wizara hiyo, Balozi Augustine Mahiga, alisema baadhi ya maafisa hao tayari wamesharejea nchini wakitokea kwenye vituo vya kazi walivyokuwapo nje ya Tanzania.

Akizungumza bila kutaja takwimu, Mahiga alisema maafisa na watumishi wengine mbalimbali wako pia katika mchakato wa kurejea nchini, baadhi wakiwa njiani na wengine wanasubiri fedha za kuwasafirisha kutoka walipo.

“Tayari kazi hiyo inaendelea. Tunavyozungumza tayari kuna wengine wengi wako hapa nchini na wengine wako njiani,” alisema Mahiga.

Akieleza zaidi, Mahiga alisema zipo baadhi ya ofisi za balozi ambazo zilikuwa na mrundikano mkubwa wa maafisa na watumishi wengine pasi na sababu za msingi.

“Kuna balozi zetu ambazo hadi sasa watumishi ni wengi sana kulinganisha na majukumu yaliyopo. Sasa tumeona ni vyema tuwapunguze na tunaendelea kutekeleza hilo kadri tunavyopata fedha za kuwasafirisha,” aliongeza Mahiga.

Ili kupata takwimu za watumishi waliopunguzwa, Nipashe ilimtafuta Msemaji wa Wizara hiyo, Mindi Kasiga, lakini kila alipopigiwa alikuwa akipokea simu yake lakini hakukuwa na majibu kutoka kwake.

Machi 4 mwaka huu, Rais Magufuli alimrudisha nyumbani aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, pamoja na watumishi wengine watano, baada ya muda wao kumalizika.

Akizungumzia hatua hiyo, Balozi Mahiga alisema kurudishwa nyumbani kwa Balozi Msuya, ni jambo la kawaida kwa sababu shughuli za kuwarudisha nyumbani mabalozi waliomaliza mikataba yao bado inaendelea.

Balozi Mahiga alisema kuna mabalozi ambao mikataba yao ya kufanya kazi nje ya nchi ni miaka mitano, lakini wamekaa zaidi ya miaka 10, hivyo serikali iko katika mchakato wa kuwarudisha nyumbani.

Mapema mwaka huu, Rais Magufuli aliwarejesha nyumbani pia Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Dk. James Msekela na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan, Dk. Batilda Salha Buriani, baada ya mikataba yao kumalizika.

Top Stories