Wapeana zamu kujifungua kisa kitanda kimoja

30Aug 2021
Pendo Thomas
KIGOMA
Nipashe
Wapeana zamu kujifungua kisa kitanda kimoja

Wajawazito katika  Kata ya Kalela Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wanapeana zamu kupanda kitandani kujifungua na wengine kulazwa chini kutokana na Zahanati ya Kalela kuwa na chumba kimoja cha wodi ya wazazi chenye kitanda kimoja.

Zahanati ya Kalela.

Njela Nikasi, mkazi wa kata ya Kalela akizungumza na Nipashe Digital leo, amesema kuna upungufu wa vitanda na wodi ya wazazi hivyo na kutaka iongezwe kwani kuna chumba kimoja  chenye kitanda kimoja hivyo  wajawazito wanao karibia kujifungua wakiwa zaidi ya mmoja  wengine hulazwa chini wakisubiri aliye kitandani ajifungue ili nae apate nafasi.

 "Wajawazito wakiwa zaidi ya mmoja wanachukua aliye karibia kujifungua anawekwa kitandani wengine wanalazwa chini huyo wa kitandani akichelewa anashushwa chini ili mwingine alazwe kitandani kujifungua"

Editha Ramadhani, mama mwenye mtoto mchanga ambaye amejifungua hivi karibuni amesema kulazwa kitandani kwa zamu na wengine  kulazwa chini wakati wakiwa na uchungu si jambo la kupendeza na wanaliona lina hatarisha usalama wa mama na mtoto.

Ameiomba serikali iboreshe miundombinu ya zahanati hiyo ikiwemo kuongeza wodi ya wazazi na vitanda hatua itakayo saidia uzazi salama.

Diwani wa Kalela, Deogratius Kabigwa amesema anatambua uwepo wa tatizo hilo linalo sababisha wajawazito kupeana zamu kulazwa kitandani na wengine chini.

Ameeleza tayari ameshachukua hatua ya kuwaailisha jambo hilo katika idara ya afya kwa utatuzi zaidi.

Top Stories