Watumishi Nida wanaswa tuhuma wizi mali mil. 15/-

19Jun 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Watumishi Nida wanaswa tuhuma wizi mali mil. 15/-

WATUMISHI saba wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), wanashikiliwa na polisi Mkoa wa Pwani kwa tuhuma za wizi wa vifaa vya mamlaka hiyo vyenye thamani ya Sh. milioni 15 ambavyo inadaiwa wameviiba na wamekuwa wakiviuza.

Kamanda Polisi wa Mkoa PWANI, Wankyo Nyigesa AKIONYESHA VITU WALIVYOKUTWA NAVYO WATUMISHI HAO.

Vifaa hivyo ni pamoja na kompyuta mpakato mbili, nyaya zake na vitambulisho vya taifa boksi moja lililokutwa likiwa na vitambulisho 15,000.

Kamanda Polisi wa Mkoa huo, Wankyo Nyigesa, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa uchunguzi, huiba vifaa hivyo na kuuza ili kujipatia fedha.

Alisema watuhumiwa hao waliiba vifaa wakati ofisi ikihamishwa kutoka ofisi ya awali iliyokuwa kwenye kiwanda cha kubangua korosho cha Tanita kilichoko Tumbi kwenda jengo jipya la Nida mjini Kibaha.

"Watumishi hawa waliteuliwa na Nida kuhamisha rasilimali vifaa kutoka ofisi hiyo ya zamani kwenda ofisi mpya za Nida, wakiwa njiani ndipo walipovichepusha na kuviuza kujipatia fedha kwa manufaa binafsi," alisema.

Kamanda Nyigesa alisema taarifa za tukio hilo zilipokelewa Nida Juni 14, mwaka huu na katika ufuatiliaji wa Jeshi la Polisi ndipo walipowakamata watumishi hao saba.

"Jumla ya thamani ya mali yote iliyoibwa ni Sh. milioni 15," alisema.

Top Stories