Kerr 'OUT' Simba

13Jan 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Kerr 'OUT' Simba
  • Mwingereza huyo amekuwa kocha wa nne kutimuliwa tangu uongozi mpya wa Simba chini Rais Evans Aveva uingie madarakani Juni 29, 2014 ...

UKIONA kunafuka moshi, ujue pana moto! Ndiyo unavyoweza kusema baada ya uongozi wa Simba kuamua kumtimua kocha wake Mkuu Dylan Kerr na kocha wa makipa, Iddi Salim kutoka Kenya.

Kerr ameondolewa Msimbazi miezi sita tu tangu alipopewa jukumu la kuinoa timu hiyo.
Baada ya kusita kwa muda, hatimaye jana uongozi wa mabingwa hao mara 18 Bara, waliamua kuvunja 'ndoa' na kocha huyo raia wa Uingereza, ikiwa ni siku mbili tu baada ya timu yao kuvuliwa ubingwa wa michuano ya Kombe la Mapinduzi ilipochapwa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Uamuzi huo pia umefikiwa ikiwa ni siku mbili tu tangu Simba iingie mkataba na kocha wa zamani wa Kagera Sugar na Coastal Union, Mganda Jackson Mayanja ambaye ulimtangaza juzi kuwa Kocha Msaidizi.
Kerr ametimuliwa baada ya kikao kilichofanyika jana makao makuu ya klabu hiyo.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zimedai kuwa kocha huyo ametimuliwa kutokana na makosa matano, ikiwamo utovu wa nidhamu dhidi ya viongozi wake na benchi la ufundi la Timu ya Taifa (Taifa Stars).
Kadhalika, amelaumiwa kwa kutokuwa tayari kushauriwa kikazi na kukataa kufanya kazi na makocha wasaidizi walioonekana kuwa na uwezo zaidi yake.
Anatuhumiwa pia kuwagawa wachezaji na kupelekea mpasuko ambao unadaiwa kuwa kiini cha timu kufanya vibaya ligi kuu.
Habari zaidi zilidai kuwa, jana kocha huyo alitishiwa kupelekwa polisi baada ya kuwaandikia meseji mbaya baadhi ya viongozi wa klabu akiwapo, msemaji Haji Manara, daktari wa timu, Yassin Gembe, meneja na mratibu wa timu, Abbas Ally Suleiman. Hata hivyo, wahusika hawakuwa tayari kuzungumzia jambo hilo wakidai wanasubiri maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu.
Kocha huyo anayelipwa mshahara wa dola 5,000 kwa mwezi ameshapewa barua yake na kesho anaondoka nchini.
Nipashe inafahamu kuwa Rais wa Simba, Evance Aveva ndiye aliyemkingia kifua Kerr kutimuliwa baada ya kipigo cha bao 1-0 ugenini dhidi ya Tanzania Prisons mjini Mbeya Oktoba 21 mwaka jana.
Ikumbukwe pia kuwa mwishoni mwa mwaka jana Aveva alikaririwa akieleza kuwa hawakuwa na mpango wa kumtimua Kerr pamoja na mwenendo mbaya wa timu ligi kuu.

KERR ANENA
Katika mahojiano maalum na Nipashe jijini Dar es Salaam jana mchana, Kerr (48), alisema hajastushwa na uamuzi huo kwa kuwa Simba haina historia nzuri na makocha inaowaajiri.
"Kama nilivyokueleza mjini Shinyanga (alipofanya mahojiano na maalum na Nipashe Desemba 27 mwaka jana), ni kweli wamenifukuza, lakini klabu hii ni ya kipekee duniani. Makocha sita na wachezaji 67 ndani ya miaka mitatu. Nimefanya kazi yangu vizuri," alisema.
"Nitajie klabu moja duniani, ambayo inaajiri na kufukuza makocha sita ndani ya miaka mitatu na kusajili wachezaji wengi namna hiyo ndani ya kipindi hicho kifupi."
Lakini, beki huyo wa zamani wa klabu za Leeds United na Reading za England pamoja na Arcadia Shepherds FC ya Afrika Kusini, aliwamwagia sifa mashabiki wa Simba kwa moyo waliomwonyesha.
"Mashabiki wa Simba ni wa kipekee Afrika. Nimekaa Afrika Kusini, niliona namna mashabiki wa Pirates na klabu nyingine walivyo. Mashabiki wa Simba wameendelea kuniunga mkono muda wote niliokaa hapa. Ninaondoka Tanzania, lakini nitawakumbuka sana," alisema.

MIAKA 17 MAKOCHA 21
Kerr, Muingereza wa pili kuzinoa klabu kongwe nchini Simba na Yanga katika miongo miwili iliyopita (1997 Steve McLennan aliinoa Yanga), amekuwa kocha wa 21 kutimuliwa Msimbazi tangu 1998 'vurugu' za kutimua ovyo makocha wakuu zilipoanza kwenye klabu hiyo.
Muingereza huyo aliyeiongoza Simba katika mechi 13 za VPL msimu huu ikishinda nane, sare tatu na kupoteza mbili ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, pia ni kocha mkuu wa nne kuinoa timu hiyo tangu uongozi wa Aveva uingie madarakani Juni 29 mwaka jana akitanguliwa na Mcroatia Zdravko Logarusic, Mzambia Patrick Phiri na Mserbia Goran Kopunovic.
Kerr pia ni kocha mkuu wa 11 kuinoa Simba katika miaka mitano iliyopita. Achilia mbali Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ na Selemani Matola, ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiinoa timu hiyo wakiwa makocha wakuu wa muda.
Tangu 2010 timu hiyo ilipita chini ya mikono ya Phiri Mbulgaria Krasmir Benziski (2011), Mganda Mosses Basena (2012), Mserbia Milovan Cirkovic (2012), Mfaransa Patrick Liewig (2013), mzawa Abdallah ‘King’ Kibadeni (2013), Mcroatia Zdravko Logarusic (2013-2014), Phiri tena (2014), Mserbia Goran Kopunovic (Januari – Mei 2015) kabla ya kutua kwa Kerr Julai mwaka jana.
Makocha walioinoa timu hiyo tangu 1998 hadi 2009 ni: Mohamed Kajole (1998), David Mwamaja (1999), Mrundi Nzoyisaba Tauzany (1999-2000), Kibadeni (2000), Syllersaid Mziray (2000), Mkenya James Siang’a (2001-2004), Phiri (2005), Mbrazil Neider dos Santos (2006), Talib Hilal raia wa Oman (2007) na Cirkovic (2008-2009).
Kerr alitua Msimbazi Julai mwaka jana na kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongezewa mmoja mwingine, iwapo angefanya vizuri Ilielezwa kuwa Muingereza huyo alikuwa anaigharimu Simba kiasi cha dola 9,000 (Sh. milioni 20) kila mwezi -- dola 6,000 (Sh. milioni 13.2) ni mshahara kwa mwezi na kiasi kinachobaki kinatumika kumlipia gharama mbalimbali zikiwamo za nyumba na usafiri.