Dawasa yatangaza ‘stop’kilio maji

25Jul 2019
Frank Monyo
Dar es Salaam
The Guardian
Dawasa yatangaza ‘stop’kilio maji
  • *Yaanza miradi yenye sura kimkakati
  • *Buza, Mwanagati, Vituka maji saa 24

MIONGONI mwa maswali ambayo kila mmoja ana jibu lake ni pamoja na: ni kiasi gani cha maji ambacho mtu anatakiwa kunywa kwa siku?  Wapo wanaosema lita tatu mpaka tano kila leo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja, akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profresa Kitila Mkumbo, kuhusu ulazaji mabomba yatakayosafirisha huduma ya maji kutoka Kibamba, Wilaya ya Ubungo, hadi Kisarawe mkoa wa Pwani.

Wengine wanadhani kiwango kinategemeana na kazi au majukumu unayoyafanya, ukiwa mpishi kwenye jiko la kuni au mkaa unahitaji mengi zaidi.

Lakini, cha msingi ni kila mtu kunywa angalau lita mbili kila siku. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani ni lazima kupata angalau glasi nane au lita mbili ambazo ni sawa na nusu galoni na kanuni hiyo inawezekana iwapo maji yanapatikana kwa uhakika.

Kwa hiyo kwa wakazi wa Dar es Salaam kwenye joto jingi na sehemu ambayo maji hupotea kwa njia ya jasho ni dhahiri kuwa maji yanahitajika mno.

Lakini maji kwa siku nyingi yamekuwa tatizo kwa wateja wa sehemu nyingi jijini hapa zikiwamo Vituka, Mwanagati na Buza ambao walikuwa na shida ya maji kwa muda mrefu. Lakini nao kuanzia sasa watarajie kupata maji safi na salama anaahidi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) Cyprian Luhemeja.

“Kwa muda mrefu wakazi wa Dar es Salaam na Pwani wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama, kwasasa adha hiyo inaelekea kuisha kwani tumedhamiria kumtua ndoo ya maji mama kichwani. Ifikapo Desemba mwaka huu. Kwa vile huduma ya maji kwa wananchi itakuwa inapatikana kwa asilimia 95.”

Luhemeja anayasema hayo baada ya miezi michache tangu kusainiwa kwa mikataba ya miradi mikubwa sita ya majisafi inayotekelezwa jijini Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani.

Anaeleza kuwa kukamilika kwake kwa wakati kutamaliza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa maeneo hayo.

Akizungumza na Nipashe wakati wa mahojiano maalaum, jijini Dar es Salaam,  Mtendaji Mkuu  Luhemeja anasema kuwa miradi hiyo mikubwa iliyosainiwa hivi karibuni ni mwendelezo wa kuondokana na kero ya maji Dar es Salaam na Pwani akieleza kuwa mikoa hiyo hasa Pwani ndiyo ukanda wa viwanda.

THAMANI YA MIRADI

Luhemeja anasema thamani ya miradi hiyo sita iliyosainiwa na Benki ya Dunia (WB) pamoja na makandarasi mbalimbali ina gharama ya Sh. bilioni 114.

Anasema kuwa miradi mitano kati ya sita iliyosainiwa inatekelezwa na Dawasa kwa kutumia fedha zake za ndani takribani Sh. bilioni 40 zitatumika.

“Dawasa hivi sasa tumeweka mikakati ya kuongeza makusanyo kwa lengo la kuendeleza na kuboresha huduma ya maji kwa kuendesha miradi ya maji kwa kutumia fedha zetu. Kati ya bilioni 114 ya miradi yote sisi tumetenga bilioni 40 kufanikisha miradi mitano ambapo mmoja kati ya miradi hiyo umesainiwa na WB,” anasema Luhemeja na kuziainisha kazi hizo kama:

MATANGI CHUO KIKUU

Luhemeja anasema kuwa mradi wa kwanza ni wa usambazaji wa maji kuanzia kwenye matangi ya Chuo Kikuu cha Ardhi mpaka Bagamoyo ambao unagharamiwa na Benki ya Dunia kwa mkopo nafuu ambao utekelezaji wake ni wa miezi 18 mpaka kukamilika.

WATAKAONUFAIKA

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, anataja sehemu zitakazofaidika na miradi hiyo itakapokamilika kuwa ni pamoja na wateja  zaidi ya 750,000. Kulingana na usanifu wao kuna wateja wapya zaidi 64,000 wa majumbani wataunganishwa na kuondokana na tatizo la maji katika maeneo ya Changanyikeni, Bunju, Wazo, Ocean by Zone, Salasala, Bagamoyo na Vikawe ambayo ni maeneo ya wilaya za Bagamoyo, Ubungo na Kinondoni.

Anaendelea kusema:" Mradi wa ujenzi wa bomba la usambazaji wa maji awamu ya pili unatekelezwa na mkandarasi na usambazaji maji utaanzia kwenye matangi ya Chuo Kikuu mpaka Bagamoyo.”

MRADI WA JETI BUZA

Ofisa Mtendaji anasema kuwa mradi wa pili ni wa kusafirisha maji kutoka Jeti hadi Buza ambapo kazi ya kulaza bomba la kilometa 1.9 imekamilika na kipande kilichobaki cha kilometa 5.6 Dawasa inaendelea kukamilisha kazi hiyo.

Anasema kuwa lengo la mradi huo ni kuhudumia wakazi wa maeneo ya Kiwalani, Vituka, Buza, Mashine namba 5-Tandika na Mwanagati ambapo wateja takribani 173.810 wa kata za Vituka na Buza watapata huduma ya maji katika awamu ya kwanza.

Mhandisi Luhemeja anasema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati iliyopangwa kutekelezwa na Dawasa kwa mwaka 2019/20 ili kukidhi agizo la serikali la kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 upatikanaji wa huduma ya maji inafikia asilimia 95 kwa maeneo ya mjini.

Anasisitiza kuwa kusainiwa kwa mikataba hiyo kutawezesha kubadilisha maisha ya wakazi wa Dar es Salaam pamoja na Pwani.

VISIMA KIMBIJI, MPERA

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, anazungumzia kuhusu visima, akisema kuwa mradi wa tatu ni wa uchimbaji wa visima 20 katika eneo la Kimbiji na Mpera ambavyo vitazalisha maji lita milioni 260 kwa siku ambapo mradi huo unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.

Anataja  mkakati wa mamlaka hiyo kuwa umejikita katika kukamilisha visima vya Kimbiji kabla ya kwenda Mpera.

“Mradi wa Kimbiji uligawanywa kwenye awamu mbili, awamu ya kwanza ilihusu uchimbaji wa visima 20 na awamu ya pili ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji kabla ya kujua wingi na ubora wa maji kutoka kwenye vyanzo vya maji chini ya ardhi kuthitibishwa kwa uhakika baada ya kuchimba,” anasema Luhemeja

Anaongeza kuwa kutokana na mkandarasi wa kwanza  aliyekuwa mgeni kushindwa kurejea kazini Dawasa imeingia mkataba na mhandisi mshauri mwingine ambaye ni mzawa ili kuendelea na kazi zilizobaki katika eneo la kipaumbele la Kimbiji ambapo amepewa muda wa miezi sita kuanzia Julai Mosi hadi  Desemba 30 mwaka huu.

MAJI KISARAWE –PUGU

Mhadisi Luhemeja anautaja mradi wa nne kuwa ni wa usambazaji wa maji kutoka Kisarawe-Pungu- Gongo la Mboto-Pugu Station-Air wing-Ukonga hadi Majohe ambao unatekelezwa  kwa gharama ya Sh. bilioni saba na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na maunganisho mapya  zaidi ya 50,000.

Anasema katika mradi huo bomba kuu litakuwa na uwezo wa kusafirisha maji lita 2,880 kwa siku ambapo wakazi zaidi ya 450,000 watanufaika baada ya kukamilika.

MAJI MKURANGA

Mtendaji Mkuu anasema  kuwa mradi wa tano utatekelezwa katika mji wa Mkuranga ambapo hali ya upatikani wa maji si ya kuridhisha kwani vyanzo vyote vya maji vimekauka na kufanya wakazi wa mji huo kutumia maji yanayotiririka kutoka kisima kilichochimbwa na Dawasa mwaka 2015 kwa ajili ya utafiti.

“Hivi sasa mtandao wa mabomba ya maji uliopo wenye urefu wa kilomita 11 unahudumia watu 4,500 kati ya watu zaidi ya 25,500 ambao ni sawa na asilimia 17.6.,” anasema Luhemeja na kuongeza:

“Mkataba wa kwanza utahusu ujenzi wa tangi la uwezo wa kuhifadhi lita 1,5000,000 na kazi zingine zitakazofanyika ni ujenzi wa kisima au “sump” na ufungaji pamp tatu za kusukuma maji kutoka kwenye kisima hadi kwenye tangi la uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa mabomba ya kupeleka maji kwenye matangi.”

Anaongeza kuwa watu wa Dar es Salaam na Pwani wanahitaji maji hivyo ni kujumu la Dawasa kuhakikisha miradi hiyo iliyosainiwa na mingine inasimamiwa vizuri kwani itakuwa mkombozi na kubadilisha taswira ya tatizo la maji.

MLANDIZI MBOGA

Mhandisi Luhemeja anautaja mradi wa sita kuwa ni wa kusafirisha maji kutoka Mlandizi au Ruvu Juu hadi Kijiji cha Mboga kilichoko Chalinze ambapo utasaidia kuondoa kero ya maji katika maeneo hayo kutokana na kuongeza kwa watu na ujenzi wa viwanda unaoendelea katika eneo la Mboga-Chalinze.

“Mradi huu wa bomba kuu unatarajiwa kusafirisha kiasi cha lita za ujazo milioni 9.3 kwa siku ambazo zitakuwa na uwezo wa kuhudumia wakazi wapatao 120 kwa siku” anasema Luhemeja.

Anaongeza kuwa maeneo ambayo yatanufaika ni maeneo ya viwanda vya ngozi, juisi za matunda, stesheni ya treni ya kisasa Vigwaza pamoja na maeneo yalio katika mpango wa viwanda.

Mbali na maeneo hayo ya viwanda, mengine ni Kijiji cha Mbonga, Chamakweza, Chahua-Lukenge, Milo, Mdaula-Ubenazomozi, Buyuni, Visezi, Vigwaza, Pingo, Pera, Bwilingu, Chalinze mjini, Chalinze mzee na Msoga.

“Ikumbukwe kuwa mradi huu pia tunatumia fedha zetu za ndani na yatajengwa maunganisho mapya ya wateja zaidi ya 18,000 eneo la Chalinze ili kuunganisha matangi yaliyopo katika eneo la mradi ili huduma ya maji iwafikie watumiaji kwa urahisi zaidi.

Top Stories