Uingereza nje Brexit

01Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Uingereza nje Brexit
  • *Tamu, chungu watakayokutana nayo

USIKU wa kuamkia leo, Uingereza imejitoa rasmi katika Muungano wa Ulaya (EU) na kuwa nchi pekee inayojitegemea katika bara hilo lenye nguvu za kiuchumi.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Borris Johnson.

Mpaka inatimiza ndoto hiyo ambayo ilipigiwa kura na idadi kubwa ya Waingereza, ndani ya miaka mitatu mawaziri wa wakuu watatu walikabiliana na joto kali mchakato huo kujiondoa, hatimaye waliamua kujiuzulu.

Waziri Mkuu wa sasa Boris Johnson, alikabiliana na vikwazo ambavyo wenzake walipitia na kushindwa, lakini yeye alifaulu na nchi hiyo sasa imeondoka rasmi.

Pamoja na furaha ya Waingereza wengi kuona wanaondoka katika muungano huo, lakini watakabiliana na kipindi cha mpito cha miezi 11 kabla ya kujitegemea.

Nini kitabadilika?

Kwa mujibu wa Shirika la BBC, wakati wa kipindi cha mpito Uingereza itaendelea kufuata sheria za EU na kutoa mchango wake wa kifedha.

Wabunge wa Uingereza kupoteza viti vyao

Nigel Farage, kiongozi wa chama cha Brexit na mwanaharakati anayeunga mkono kampeni ya Uingereza kujiondoa katika Muungano wa Ulaya, atakuwa mmoja wa wabunge 73 wa Uingereza katika bunge la Ulaya watakaopoteza viti vyao.

Hii ni kwa sababu Brexit ikifanyika Uingereza italazimika kujiondoa katika taasisi za kisiasa za EU na mashirika yake.

Uingereza itafuta sheria ya Uingereza katika kipindi cha mpito, Mahakama ya Haki ya Ulaya itaamua jinsi sheria za EU zitakavyotekelezwa.

HAIRUHUSI MIKUTANO EU

Waziri Mkuu wa Ungereza, Boris Johnson, atapewa mwaliko maalum endapo atataka kuungana na viongozi wengine katika kongamano la baraza la Ulaya siku zijazo.

Mawaziri wa Uingereza pia hawatahudhuria mikutano ya mara kwa mara ya muungano huo ambayo inaamua masuala kadhaa muhimu.

MASUALA YA KIBIASHARA

Uingereza itaweza kuanza mazungumzo ya kibiashara na nchi mbalimbali duniani kuhusu kuweka taratibu mpya wa kununua na kuuza bidhaa na huduma.

Haikuruhusiwa kufanya mazungumzo na nchi kama Marekani na Australia wakati ikiwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Kambi inayounga mkono kujitoa kwa Uingereza inasema kuwa itakuwa na uhuru wa kuweka sera zake za kibiashara kwa ajili ya kuinua uchumi wake.

Kuna umuhimu wa kujadiliana na EU kuhusu kukubaliana kibiashara kati ya Uingereza na EU.

Ikiwa itafikia makubaliano ya kibiashara, hawataweza kuanza mpaka kipindi cha mpito kitakapokamilika.

PASIPOTI ITABADILISHWA RANGI

Akitangaza mabadiliko hayo mwaka 2017, Waziri wa Uhamiaji, Brandon Lewis, alisifia kurejea kwa pasipoti ya kipekee za rangi ya bluu na dhahabu, ambazo zilitumika mwaka 1921.

SARAFU YA BREXIT

Karibu sarafu milioni 50 zilizo na alama ya tarehe "Januari 31" na iliyoandikwa: "Amani, mafanikio, urafiki na mataifa yote", itaanza kutumika Ijumaa.

Sarafu hizo zimepokelewa kwa hisia mseto, huku wafuasi wanaotaka kubaki wakisema hawaikubali.

Serikali ilikuwa imepanga kuzindua sarafu hiyo Oktoba 31, tarehe ya awali iliyowekwa kwa ajitoa Brexit.

Hata hivyo sarafu hizo ziliyeyushwa na kuundwa tena baada ya muda wa mwisho kurefushwa.

IDARA BREXIT KUFUNGWA

Jopo la mashauriano ya Uingereza na EU limekuwa likiongoza mchakato wa Brexit litavunjwa.

Idara inayoendesha mchakato wa Uingereza kujiondoa Muungano wa Ulaya iliundwa na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Theresa May, mwaka 2016.

Kwa mazungumzo yatayofuata, timu ya mashauriano ya Uingereza itakuwa na makao yake Downing Street.

UJERUMANI HAITABADILISHANA WAFUNGWA NA UINGEREZA

Haitawezekana kuwarejesha Uingereza watu wanaoshukiwa kuwa wahalifu waliotorokea Ujerumani.

Katiba ya Ujerumani hairuhusu raia wake kushtakiwa katika nchini nyingine isipokuwa mataifa ya Muungano wa EU.

"Hatua hii haiwezi kufanyika tena baada ya Uingereza kujiondoa katika Muungano wa EU," Msemaji wa Wizara ya Haki ya Ujerumani aliambia BBC.

Haijabainika kama udhibiti huo utahusisha nchi zingine za muungano huo, Slovenia, kwa mfano, inasema hali hiyo ni ya kuchanganya, lakini Tume ya Ulaya haikuweza kutoa tamko lolote kuhusu suala hilo.

Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza inasema waranti ya kukamatwa ya Ulaya itaendelea kuzingatiwa katika kipindi cha mpito.

MAMBO HAYATOBADILIKA

Katika kipindi cha mpito vitu vingi vitasalia kama kawaida hadi tarehe 31 mwezi Desemba 2020:

Usafiri wa ndege, boti na treni zitaendelea kuhudumu kama kawaida.

Linapokuja suala la udhibiti wa pasipoti, katika kipindi cha mpito, raia wa Uingereza wataruhusiwa kupanga foleni katika eneo lililotengewa raia wa mataifa ya EU.

Leseni halali zitaendelea kutumika na kadi za bima zinazotolewa na serikali kwa raia wa Uingereza ili wapate huduma za matibabu wakiwa wagonjwa au wakipata ajali.

Uhuru wa kusafiri utaendelea kuzingatiwa katika kipindi cha mpito, kwa hivyo raia wa Uingereza wataweza kuishi nchini humo na kufanya kazi nchi yoyote ya EU kama wanavyofanya sasa.

Raia wa Uingereza wanaoishi katika mataifa wanachama wa Muungano wa Ulaya wataendelea kupokea malipo yao ya uzeeni na pia nyongeza yao ya kila mwaka.

Pia Uingereza itaendelea kuchangia bajeti ya EU wakati wa kipindi cha mpito, itaendelea kufadhiliwa.

Biashara kati ya Uingereza na Muungano wa Ulaya itaendelea bila malipo yoyote ya ziada au kubuniwa kwa sheria mpya za forodha.

Top Stories