Hatua hiyo inaanza kwa kupokea maoni ya wanachama wake ili kupata hisia zao kuhusu mustakabali wa mafanikio, matatizo na changamoto za juhudi hizo, anatangaza Mwenyekiti wa chama Juma Duni Haji.
Anaeleza kuwa kimeridhia kupokea maoni kwa wananchama kuhusu kazi hiyo ya kisiasa baada ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi kumteua Thabit Idarusi Faina, kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), jambo analodai linazusha mjadala mkubwa ndani ya chama hicho na hivyo kutaka kusikia wanachama wana maoni gani.
Anasema wanachokilalamikia ni yale yaliyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2020 wakati Faina akiwa Mkurugenzi wa Uchaguzi ZEC, hivyo yasijitokeze tena katika uchaguzi huo ambao ACT-Wazalendo hawayakubali.
Anasema uchaguzi ndiyo kiini cha mifarakano Zanzibar hivyo ni lazima kutayarisha uchaguzi huru, wa haki na unaokubalika na anayeshinda atangazwe bila kuwa na kona kona au mazingira yanayolalamikiwa.
Mwenyekiti Duni akizungumza juzi na wazee wa ACT- Wazalendo visiwani hapa, anasema lazima wanachama kulijadili kwa uwazi, undani na kulitafakari vya kutosha kuhusu maridhiano ya kisiasa Zanzibar ambayo chama hicho ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Niwaombe wanachama msiogope kutoa mawazo yenu mnayoyaamini, kuhusu mustakabali wa maridhiano ya kisiasa na mawazo ya wengi ndiyo yatakayoridhiwa na chama”anasema Duni.
Mwenyekiti huyo anasema chama hicho kimeridhia maridhiano hayo ni miaka miwili imesalia hivyo wanahitaji kufanya tathmini kwa sababu njia ya maridhiano ndiyo pekee itayoifikisha kwenye kujenga nchi kwa salama na amani.
Anasema lengo la maridhiano hayo kuyatafutia ufumbuzi wa matatizo ya kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa visiwani humo.
Anawaeleza kuwa licha ya madhila na mateso mbalimbali waliyopitia katika chaguzi zilizopita lakini ifike mahala kusahau yaliyopita na kushikamana kwa ajili ya Wazanzibari wote na taifa zima.
“Yaliyopita si ndwele tugange yajayo Wazanzibari tutakaposhikamana na kuridhiana amani na usalama wa nchi utapatikana. Upendo na uvumilifu na kusameheana ni muhimu ili kuponya majeraha,”anasema.
Aidha, anasisitiza kuwa bila ya maridhiano hakuna maendeleo hivyo ni lazima kupendana, akiongeza kuwa kwenye mfarakano huwezi kupata maendeleo na muwekezaji akijua nchi fulani wanagombana hapeleki rasilimali zake, kwa vile anafahamu hakuna tija.
“La msingi ndugu zangu na CCM wananisikia maridhiano na sisi hatutokuwa wa mwanzo au wamwisho, Marekani na Uingereza waligombana lakini leo ni marafiki, Wajapani na Waamerika kadhalika walipigana lakini leo ni rafiki na wapo wanaishi,”anakumbusha Duni.
Pia anatoa mfano wa mapigano ya Afrika Kusini ambayo kulikuwa na mapingano kati ya Wazungu na weusi, lakini imefika mahali wamemaliza tofauti zao na sasa ni mfano wa nchi zilizoendelea barani Afrika ambazo hazina ugomvi.
Anasema miaka 17 Msumbiji walikuwa wanapigana wenyewe kwa wenyewe lakini pia Kenya hivi karibuni walipigana na kuuana leo kuna maridhiano na wamejenga umoja na kufanyakazi pamoja kuendeleza nchi yao.
“Wazanzibari na mwafaka bado tunafikiria eti tukigawana tutafanikiwa, haiwezekani kufanikiwa kwa mifarakano, ”anasisitiza kuwa cha muhimu ni maridhiano na uvumilivu wa kisiasa.
ACT WAUNGWA MKONO
Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima AFP, Said Soud, anatangaza kuungana na ACT- Wazalendo kupinga Faina kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa ZEC ili kuiepusha nchi kuingia katika vurugu za uchaguzi.
“Ili Rais Mwinyi afanikishe kutafuta suluhisho la mwafaka litakalojenga imani za Wazanzibari amwondoe Faina na atakayemweka si vibaya akipigiwa kura na vyama vya siasa ili kuonyesha uwepo wa maridhiano ya kweli.”
“Ikiwa hajaanza kazi watu wanamkataa je akianza majukumu itakuwaje? Demokrasia haitaki mivutano na hasa pale kiongozi mkuu anapoahidi atafanya maridhiano na kuyaendeleza sasa maridhiano yanaanza katika ngazi ya chini halafu yanapanda juu,”anasema Soud.
Mwenyekiti huyo anasema Rais Hussein Mwinyi, anashauriwa na ingependeza kama atakuwa tayari kusikiliza maoni ya vyama vya siasa hasa vile vyenye nguvu zaidi na vilivyothubutu kuingia katika serikali yake na kuunda SUK.
Anaeleza kuwa katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2020 yeye alinyimwa kura wakati huo Mkurugenzi wa Uchaguzi ZEC akiwa Faina hivyo hata yeye hawezi kumhitaji mkurugenzi huyo.
TADEA YAONYA ACT
Juma Ali Khatib ni Mwenyekiti wa Chama cha Ada-TADEA anayesema maridhiano ya kisiasa hayajatoa uhalali wa viongozi wa chama cha ACT-Wazalendo kuingilia madaraka ya Rais wa Zanzibar ambayo yapo kwa mujibu wa katiba.
Anafahamisha kuwa viongozi wa chama hicho hawatakiwi kumpangia kazi Rais ambaye majukumu yake yako kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi ambapo halazimiki kupokea ushauri wa mtu katika shughuli za utendaji wa kazi zake za kila siku.
''Mimi nawasihi wanasiasa wenzangu kuacha kufanya hivyo kuingilia majukumu ya Rais, ameonyesha nia ya dhati ya kutekeleza maridhiano ya kisiasa ambayo lengo lake ni kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar aachwe ''anasema Khatibu.
Anaungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu UVCCM Zanzibar, Mussa Haji Mussa, anasema kitendo cha kuingilia majukumu ya Rais Mwinyi katika eneo la uteuzi ni sawa na kuingilia katiba pamoja na kudharau maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa ambayo serikali imeonyesha nia ya kuyatekeleza kwa vitendo.
Anasema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake maridhiano yametekelezwa kwa vitendo ikiwamo Rais kufanya juhudi za ziada za kuunda kikosi kazi kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi mambo mahususi kwa siasa za Zanzibar.
Anaongeza kuwa masuala ya kuteua mtendaji pamoja na kutengua yapo katika mamlaka ya Rais wa Zanzibar ambayo hakuna kiongozi mwenye uwezo wa kuhoji maamuzi hayo.
''Rais akiteua na kutengua hakuna kiongozi mwingine wa kuhoji maamuzi hayo na hili ni kwa mujibu wa katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hili la kumshurutisha maamuzi yake linakwenda kinyume na katiba''anakumbusha Musa.