Yanga ijipange kuing'oa APR Afrika

29Feb 2016
Mhariri
Nipashe
Yanga ijipange kuing'oa APR Afrika

YANGA imefanikiwa kutinga hatua ya kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kuing'oa timu ya Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0.

Mabingwa hao mara 25 wa Tanzania Bara walishinda 1-0 ugenini nchini Mauritius wiki mbili zilizoita kabla ya kuitungua tena timu hiyo kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi.

Kwa matokeo hayo, sasa Wanajangwani watakutana na APR ya Rwanda ambayo imewang'oa Mbabane Swallows ya Swaziland.

Mechi ya kwanza itachezwa kati ya Machi 11 na 12 kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali, Rwanda wakati mchezo wa marudiano utachezwa wiki moja baadaye jijini Dar es Salaam.

Tukiwa wadau namba moja wa michezo nchini, Nipashe tunaipongeza Yanga kwa kuvuka hatua ya awali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Tunaamini kuwa ubora wa kikosi, utulivu ndani ya uongozi na uhusiano mzuri baina ya makocha, wachezaji na uongozi ndivyo vitu vilivyochagiza mafanikio ya klabu hiyo ya Jangwani.

Hata hivyo, tunatoa rai kwa uongozi wa Yanga na benchi la ufundi la timu hiyo kuanza maandalizi mapema ya mechi mbili zijazo za hatua ya kwanza dhidi ya APR.

APR ni miongoni mwa timu bora kwenye ukanda wa Cecafa wa Afrika Mashariki na Kati ndiyo maana haijashangaza kuona timu hiyo inashinda kwa idadi kubwa ya mabao (4-1) dhidi ya Mbabane Swallows jijini Kigali, Rwanda juzi.

Timu hiyo iliyopanzishwa Juni 1993, ina mataji matatu ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati iliyoyatwaa 2004, 2007 na 2010 baada ya kupoteza katika fainali mbili za michuano hiyo 1996 na 2000.

APR pia imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda mara 13 na ina uzoefu mkubwa wa michuano ya Afrika ikishiriki Ligi ya Klabu Bingwa mara 10 na Kombe la Shirikisho mara tatu licha ya kushindwa kuvuka raundi ya kwanza.

Kutokana na uzoefu mkubwa ilionao APR, tunaona kuna haja wawakilishi wa Tanzania waliobaki kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwaka huu, Yanga kuanza mapema maandalizi ya mechi mbili zijazo dhidi ya timu hiyo ya jeshi.

Tunafahamu kikosi cha Yanga tayari kimekimbilia mafichoni kujiandaa kwa mechi ya Jumamosi dhidi ya Azam FC, lakini ni vyema maandalizi hayo yakaenda sanjari na kuisoma APR nje na ndani ya uwanja ili kubaini mbinu na ubora wa timu hiyo ya Ligi Kuu ya Rwanda.

Yanga imekuwa haifiki mbali katika michuano ya Afrika iking'olewa na Al Ahly na Etoile du Sahel misimu miwili iliyopita. Bila maandalizi mazuri kabla ya mechi mbili zijazo dhidi ya APR, tunaamini msimu huu pia utakuwa mbaya kwa Wanajangwani.

--------------

Top Stories