Fifa yamfungia Malinzi miaka 10

12Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
ZURICH, Uswisi
Nipashe
Fifa yamfungia Malinzi miaka 10
  • ***Ni kwa matuimizi mabaya ya fedha shirikisho hilo, pia atakiwa kulipa faini Sh. bilioni moja huku...

Shirikisho la Soka duniani (Fifa), limemfungia kwa miaka 10, Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi kwa matumizi mabaya ya fedha za shirikisho hilo.

Jamal Malinzi.

Aidha, kifungo hicho pia kinakwenda sambamba na Malinzi kulipa faini ya dola 503,000 sawa na Sh. bilioni 1.1 za Tanzania kwa Fifa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Fifa, imeeleza Malinzi alipokea dola 528,000 (Sh. bilioni 1.2)kwa zaidi ya miaka minne kwa madai ya kulipia mikopo ambayo "ilikosa udhibitisho ama maelezo sahihi"

Pia ilieleza Malinzi alipokea dola  55,000 (Sh. milioni 126. 3) fedha ambazo zilikuwa zawadi kwa timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya miaka 17 (Tanzania U-17) kwa kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika iliyofanyika Gabon 2017.

FIFA imesema Malinzi alikuwa mjumbe wa Kamati yake ya Maendeleo - ya kutenga pesa za miradi yote duniani - kipindi akiwa katika jukumu hilo la mchezo wa haki na kamati ya uwajibikaji kijamii kuanzia mwaka 2013-17 wakati akichukua fedha hizo.

ALIPO MALINZI

Kwa sasa Malinzi na wenzake, aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa na Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawayo Mwanga (27) wapo rumande wakikabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 213 ya mwaka 2017, washtakiwa Malinzi, Mwesigwa na Nsiande walikosa dhamana kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.

Kesi hiyo ilikuwa na mashtaka 30, lakini ilipofikia katika uamuzi wa kama washtakiwa wana kesi ya kujibu ama la walipunguziwa mashtaka 10 kati ya 30 yaliyokuwa yakiwakabili baada ya Jamhuri kushindwa kuonyesha kama washtakiwa wana kesi katika makosa hayo.

Mahakama hiyo iliwakuta wana kesi ya kujibu washtakiwa hao kwa mashtaka 20 yaliyobakia baada ya Jamhuri kuonyesha kwamba wana kesi, hivyo walijitetea wenyewe bila kuita na mashahidi. Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo iliyokuwa na mashahidi 15 na vielelezo tisa.

Aidha, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Novemba 7, mwaka huu ilipiga kalenda kutoa hukumu ya kesi hiyo ya Malinzi na wenzake mpaka Novemba 21, mwaka huu.

 

 

 

Top Stories