Kaheza awazia soka la kimataifa

19May 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kaheza awazia soka la kimataifa

STRAIKA wa Polisi Tanzania, Marcel Kaheza, amesema bado anafikiria kucheza tena soka nje ya nchi, licha ya kurejea nchini akitokea Kenya ambako alikuwa akicheza soka la kulipwa kwenye klabu ya AFC Leopards ya Kenya.

STRAIKA wa Polisi Tanzania, Marcel Kaheza:PICHA NA MTANDAO

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaheza anayeichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Simba, amesema mkataba wake na Polisi Tanzania unamalizika mwishoni mwa msimu huu na sasa kama si kubaki na timu hiyo, basi ataangalia changamoto nyingine nje ya nchi.

"Ni kweli kwa sasa namalizia mkataba wangu, tayari nina mazungumzo na timu yangu ya Polisi Tanzania kama wakifanikisha kunibakisha, lakini kama sivyo, basi siangalii hapa, naangalia nafasi nyingine ya kwenda kucheza soka la kulipwa," alisema mchezaji huyo ambaye Simba ilimsajili akitokea Majimaji ya Songea.

Straika huyo ambaye kwa sasa ana mabao sita Ligi Kuu, aliongeza: "Bado nina umri mdogo na ndoto zangu ni kutoka hapa na kwenda kucheza soka kwenye klabu mbalimbali kubwa barani Afrika na kwingineko, uzuri ni kwamba tayari nimeshatoka kucheza soka nje ya nchi, najua changamoto za huko, hivyo nitakabiliana nazo," alisema.

Kaheza ambaye alianzia soka kwenye kikosi cha vijana cha Simba kabla ya kwenda Majimaji ya Songea, alisajiliwa tena na Simba mwaka 2018, lakini kutokana na wakati huo klabu hiyo kuwa na malengo makubwa zaidi kwa kusajili wachezaji kama Meddie Kagere, Claotus Chama na wengine, alikosa nafasi na mwaka huo huo akapelekwa klabu ya AFC Leopards ya Kenya kwa mkopo.

Mwaka mmoja baadaye alirejea nchini na kujiunga tena kwa mkopo klabu ya Polisi Tanzania ambayo anamaliza mkataba wake pindi Ligi Kuu Tanzania Bara itakapomalizika, hivyo kuwa na uhuru wa kuchagua kituo kingine kiwe ndani ama nje ya Tanzania.

Top Stories