Simba baba lao!

24Feb 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba baba lao!
  • Yaichapa Al Ahly 1-0 na kuongoza katika Kundi A…

SIMBA baba lao. Hivyo ndivyo inavyoweza kuelezwa baada ya mabingwa hao wa Tanzania mara tatu mfululizo sasa, kuwafunga mabingwa wa Afrika, Al Ahly kutoka Misri bao 1-0.

Winga wa Simba, Luis Miquissone (katikati), akijiandaa kupiga shuti huku golikipa wa Al Ahly, Ahmed El Shenawy (kushoto), akifanikiwa kuondoa hatari kwenye lango lake katika mechi ya Kundi A ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Simba ilishinda bao 1-0. PICHA: JUMANNE JUMA

Katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, raia wa Msumbiji, Luis Miquissone, maarufu kama Konde Boy, ndiye aliyefunga bao hilo pekee ambalo limeiwezesha Simba kufikisha pointi sita na kukaa kileleni mwa Kundi A la michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Miquissone alifunga bao hilo dakika ya 31 baada ya kuupata mpira nje ya eneo la hatari, akawazungusha mabeki wa Al Ahly na kuachia shuti kali la mguu wa kushoto kisha mpira kugonga mwamba wa juu, ukatinga wavuni.

Kwa ushindi huo, Simba imeendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi yoyote kwenye ardhi ya Tanzania, ikicheza na timu za Afrika Kaskazini, maarufu kama Waarabu kwenye historia ya klabu hiyo.

Kama vile haitoshi, inakuwa mara ya tatu kuifunga Al Ahly nchini Tanzania. Mara  ya kwanza ikiwa mwaka 1985 ikishinda mabao 2-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba,  Mwanza na mara ya pili Februari 12, 2019 ikishinda bao 1-0 kwenye michuano kama hii hatua ya makundi, zilipokuwa kwenye Kundi D.

Lakini inaendeleza rekodi yake safi ya kutopeteza mechi yoyote ya kimataifa kwa miaka saba sasa ikicheza nchini Tanzania. Mara ya mwisho ilifungwa  kwenye Kombe la Shirikisho la Afrika, Februari 17, 2013  dhidi ya Recreativo do Libolo ya Angola.

 

Katika mechi ya jana, kila timu ilionyesha uwezo wa hali ya juu, huku zikishambuliana kwa zamu, lakini Simba ikikosa mabao mengi.

Dakika ya sita tu, Luis Miquissone nusura aipatie Simba bao, kama si kuukokota sana mpira na kusukumwa kidogo na beki wa Al Ahly kabla ya kuanguka na mpira kuwahiwa na kipa Ahmed Al Shenawy.

 

Shomari Kapombe alichelewa kuuwahi mpira uliotangulizwa mbele yake, akiwa kwenye eneo la hatari na kipa Shenawy akauwahi.

Dakika ya 16, Kahraba aliwahadaa mabeki wa Simba, Joash Onyango na Paschal Wawa, akaachia shuti kali lililopita juu ya lango la Simba.

Wachezaji wa Simba walipata kigugumizi cha kuuweka mpira wavuni, uliopigwa na Miquissone ukizua kizaazaa kwenye lango la Al Ahly, kabla ya mabeki wa timu hiyo kuufagia na kuondosha hatari.

Dakika moja baadaye, Walter Bwalya aliruka juu na kuupiga kichwa mpira uliotoka nje kidogo ya lango la Simba. Kipa El Shenawy, aliwaokoa Al Ahly dakika ya 39, alipopangua shuti la Chriss Mugalu na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko, Simba ikiwatoa Thadeo Lwanga aliyeumia na kuingia Erasto Nyoni, Meddie Kagere akichukua nafasi ya Mugalu, na Francis Kahata nafasi ya Miquissone, Clatous Chama akitoka na ikachukuliwa na Kennedy Juma.

Mzamiru Yassin aliikosesha Simba bao dakika ya 71 baada ya shuti lake kuzuiwa na beki, Yasser Ibrahim na kuwa kona.

Dakika tano za mwisho, Al Ahly ilicharuka na kukosa mabao mawili ambayo yangeleta majonzi kwa Watanzania. Dakika ya 85, Mohamed Wahid aliikosesha timu yake bao, alipopiga mpira ulitoka nje ya lango.

Aishi Manula aligeuka kuwa shujaa dakika moja kabla mechi kumalizika, alipopangua kwa ustadi shuti la Mahmoud Kahraba.

Aidha, katika mechi nyingine ya kundi hilo iliyochezwa jana, AS Vita ikiwa ugenini jijini Khartoum nchini Sudan ilipata ushindi wa mabao 4-1, dhidi ya wenyeji El Merrik.

Top Stories