Niyonzima amfukuzisha Tiboroha Yanga

24Jan 2016
Lete Raha
Niyonzima amfukuzisha Tiboroha Yanga

IWAPO Klabu ya Yanga isingemrudisha kazini kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, pengine ingeweza kuingia hasara ya kumlipa kiungo huyo Mnyarwanda fedha dola 71,175 (Sh. milioni 142) kama gharama ya fidia ya kuvunja mkataba.

Haruna Niyonzima

Licha ya uongozi wa klabu hiyo kupitia kwa aliyekuwa katibu, Jonas Tiboroha, kusema wazi kuwa wamemfukuza kiungo huyo, hali imebadilika kwani uliamua kutengua hali hiyo na kumrejesha kazini huku ikidai wazi kuwa maamuzi hayo yalimuudhi Tiboroha ambaye awali aling'ang'aniza kiungo huyo atimuliwe kutokana na kutoheshimu mkataba wake.
Chanzo cha ndani kiliieleza LeteRAHA, “Niyonzima ndiye chanzo cha Tiboroha kujiuzulu na kwamba katibu huyo amewaambia watu wa karibu kuwa hajafurahishwa na kitendo cha kiungo huyo kurejeshwa ilhali hakuwa na sababu kutokana na nidhamu yake kuwa mbovu.
"Dkt Tiboroha ni msomi na anayefahamu vyema sheria za kazi, kujiuzuu kwake inatokana na viongozi wengine kushinikiza Niyonzima afutiwe adhabu ya kuvunjiwa mkataba na kurejeshwa kwenye timu kitu ambacho kilimkera Tiboroha na kudai kuwa hawezi kuendesha mambo kienyeji kwa utaratibu usioeleweka.”
Mapema jana Tiboroha alijiuzulu kwa kuwasilisha barua kwa mwenyekiti wa timu hiyo.
Tiboroha alisema kuwa alichukua uamuzi huo ilia apate muda zaidi wa kufanya shughuli zake za Uhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Mimi ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitivo cha Elimu ya Viungo (PE), na kwa kuondoka Yanga maana yake napata wasaa mzuri wa kumtumikia mwajiri wangu, UDSM, lakini pia napisha wengine waweze kufanya kazi," alisema.
Kwa upande mwingine, Tiboroha alipoulizwa kuhusu kuwa na mawasiliano mabaya na baadhi ya viongozi alisema; “Nilichoandika katika barua yangu ya kujiuzulu ndiyo sababu za msingi, kikubwa ninawapisha watu ambao wanaweza kuiongoza vizuri Yanga kuliko mimi.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Isaac Chanji, alisema kuwa Tiboroha ameondoka Yanga kutokana na tuhuma mbalimbali zilizokuwa zinamkabili mbele ya Kamati ya Utendaji, ikiwamo utendaji usioridhisha na kupoteza uaminifu.
Miongoni mwa tuhuma ambazo zimemtoa Tiboroha Yanga ni pamoja na kuajiri watu bila ridhaa ya Kamati ya Utendaji, kusafiri kwenda Ghana kwenye kongamano la Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) bila ridhaa ya mwajiri wake, huku akiaga ameenda kwao Kigoma kwa matatizo ya kifamilia.
Tiboroha aliingia Yanga Desemba mwaka 2014 akichukua nafasi ya Benno Njovu aliyeondolewa kwa tuhuma mbalimbali. Aliingia Yanga akitokea Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama Ofisa Maendelezo ya Ufundi.

Top Stories