Natamani upinzani wa muki hawa

12Jun 2016
Barnabas Maro
Lete Raha
MZEE YANGA
Natamani upinzani wa muki hawa

MUKI ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kifedha. Natamani kuona muki wawili wakileta upinzani kwa Said Salim Bakhresa katika maendeleo ya vilabu nchini.

Mohamed Dewji ambaye kuna wakati alikuwa mfadhili wa Simba, lakini akajiondoa. Kwa nini, usiniulize kwani lililopita hupishwa. Baadaye ‘alinunua’ timu inayoitwa mpaka leo African Lyon.

Baadhi ya watu hawakujua; lakini ‘lyon’ ni neno la Kifaransa yaani simba kwa Kiswahili. Ni tofauti na inavyoandikwa kwa Kiingereza ‘lion’ lakini maana ni ileile -- simba. Kwa sababu azijuazo (MO), akaiuza.

Tuachie hapo kwani alikuwa na sababu zake. Wahenga watwambia “usilolijua ni usiku wa kiza.” Hatujui kilichomfanya aiuze.

Miezi ya karibuni, alijitokeza hadharani kutaka kuinunua klabu ya Simba ili amiliki asilimia 51 za hisa na zilizobaki zimilikiwe na klabu. Akaahidi endapo atakubaliwa, ataibadili Simba iwe ya kisasa kutokana na maendeleo atakayofanya.

Kwamba angefanya huduma zote zinazohusu maendeleo ya kandanda - viwanja, kusajili wachezaji nguli, kulea na kukuza vipaji vya wachezaji wadogo wa baadaye.

Baadhi ya wanachama na mashabiki wa Simba na Yanga wana tafsiri tofauti ya ‘maendeleo.’ Kwao, ‘maendeleo’ ni mojawapo kuifunga nyingine ili watambe mitaani na kwenye magenge ya kahawa, basi!

Mohamed Dewji alipopendekeza ainunue klabu ya Simba, wachumia tumbo wakasema: “hapana … tukale wapi?” Wakaupinga mpango huo. Sasa baada ya Simba kufanya vibaya kwa misimu minne mfululizo, suala la Dewji limeibuliwa.

Wasiotaka kusikia habari hiyo ni wale wanaonufaishwa na klabu. Wanaotaka ni waliochoshwa na maendeleo duni ya timu na klabu kwa jumla. Ni patashika nguo kuchanika, lakini mwenyewe (Dewji) katulia tuli kama maji mtungini.

Yanga kuna muki wao ambaye amekuwa tegemeo kubwa kwao. Usajili, mishahara ya wachezaji, benchi la ufundi na safari za ndani na n-nje ya nchi hutegemea mfuko wake. Wapo wanaosaidia hapa na pale kuokoa jahazi lisende mrama.

Kuna wakati muki wa Yanga alipendekeza kwa wanachama klabu iwe kampuni akaahidi kuwalipia wanachama hisa ili ijitegemee. Wanaotaka kujinufaisha kwa kivuli cha Yanga wakakataa.

Ukiangalia, hakuna msaada wowote wanaotoa kusaidia maendeleo ya klabu. Tatizo la vilabu hivi vikongwe na maarufu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na kwingineko, ni kukosa ari (moyo wa kutaka kufanya jambo bila ya kushindwa; shauku) ya maendeleo.

Kwa nyakati tofauti Yanga na Simba zilipata viongozi wenye dira ya maendeleo, lakini walishindwa kutokana na wanachama ‘magoli’ kutotambua umuhimu Wanachama na mashabiki wa aina hii huwafanyia fujo viongozi wenye malengo ya maendeleo wakidai waachiwe ‘vilabu vyao!’ Ukiwauliza wana mchango gani katika vilabu vyao, hubaki kukuangalia kwa mshangao kama mtu aliyetoka sayari nyingine!

Kwa ufinyu wa nafasi, nasubiri kwa hamu kuwaona muki wa Azam, Simba na Yanga wakishindana kuvifanya vilabu hivyo kuwa vya kimataifa hasa. Wataweza au angalau kuikaribia Azam? Muda ndiyo utakaojibu.

[email protected]
0715/0784 33 40 96